December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahariri wanolewa uchechemuzi marekebisho sheria za habari

Spread the love

 

BAADHI ya wahariri nchini Tanzania, wamepewa mbinu za kufanya uchechemuzi kuhusu marekebisho ya Sheria zinazohusu masuala ya habari. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mbinu hizo zimetolewa leo tarehe 22 Oktoba, 2022 katika mafunzo kwa wahariri kuhusu mikakati ya uchechemuzi wa marekebisho ya sheria hizo, yaliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania Kwa kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo Taasisi za Internews, ICNL, USAID na Mseto.

Mtoa mada katika mafunzo hayo, Tumaini Mbibo, amewataka wahariri na wadau wengine katika tasnia ya habari, kuvifahamu vyema vifungu kandamizi vya sheria hizo, ambavyo wanataka virekebishwe au viondolewe kabisa.

Amesema wakivijua vifungu hivyo wataweza kuainisha athari zake pamoja na kupanga mkakati wa kuhamasisha zirekebishwe.

“Ukizijua utajua unataka mabadiliko ya sheria zipi, ngapi kati ya hizi Tano, kama unataka mbili zirekebishwe ndani ya muda gani, miaka mitano au mitatu ya utawala fulani. Uongozi ukipinduka tunataka kusikia kitu hiki kimebadilishwa Ili tumpime kama ndani ya miaka mitano sheria hizi zimebadilishwa,” amesema Mbibo.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile

Mtoa mada huyo, amewataka wahariri kuweka ajenda mahususi zenye ujumbe utakaoshawishi mamlaka husika kurekebisha Sheria hizo. Pia, amewataka kutengeneza muungano wa wadau katika sekta nyingine, ambao wanahusika katika mchakato wa marekebisho hayo hayo kama wabunge, mawakili.

“Tuwe tunaboresha jumbe zetu, huwezi kutengeneza ujumbe ule ule Kwa mbunge anayepitisha sheria, jaji anayeamua kesi kuleta marekebisho ya Sheria au kwa mtu anayeandaa muswada wa sheria,” amesema Mbibo na kuongeza:

“Ziko mbinu nyingi za aina mbalimbali ambazo kufikia wafanya maamuzi, inaweza Kwa kutumia barua, ushaiwishi au kama nguvu unayo kuwakutanisha wajumbe wa kamati wa jambo linalokuhusu, watakusikia na watakusaidia.”

Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amewataka wadau wa habari hususan waandishi wa habari kuongeza juhudi katika shughuli za uchechemuzi wa marekebisho ya Sheria, Kwa kuandika habari nyingi na kufanya vipindi vya midahalo katika vipindi vya runinga, inayohusu masuala hayo.

“Tutaendelea kuongeza nguvu mara kwa mara, tukimaliza kuweka mikakati ya uchechemuzi tuwe na kipindi cha mubashara angalau Novemba, Januari, Machi, cha mdahalo. Pia, tunahitaji dhamira tuchapishe habari nyingi zaidi,” amesema Balile.

Miongoni mwa sheria ambazo wadau wa habari wamependekeza zifanyiwe marekebisho ili kuondoa vifungu kandamizi Kwa uhuru wa habari ni, Sheria za Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015, Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya 2016 iliyofanyiwa marekebisho 2017 na Sheria ya Takwimu.

Miongoni mwa vifungu vinavyolalamikiwa ni vile vinavyotoa mamlaka kwa watendaji wa Serikali dhidi ya vyombo vya habari hususan katika masuala ya utoaji leseni, adhabu, matangazo na tafsiri ya mwandishi wa habari.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, Kwa Sasa Iko katika mchakato wa kupokea na kujadili mapendekezo yaliyotolewa na wadau kuhusu marekebisho ya sheria hizo.

Hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema mchakato huo unaendelea vizuri na kwamba taarifa itatolewa Kwa umma pindi utakapokamilika.

error: Content is protected !!