September 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahariri wamkaanga Makunga na wenzake

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Theophil Makunga

Spread the love

WAHARIRI wa vyombo mbalimbali vya habari wametoa onyo kali kwa uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwa kudhalilisha jukwaa hilo pamoja na tasnia nzima ya habari hapa nchini, anaandika  Hellen Sisya.

Katika kikao chao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, wahariri hao wamekubaliana kwa pamoja kuwapa onyo kali viongozi wa TEF, na kuwataka kutokurudia tena kosa hilo.

“Baada ya kutafakari na kutathmini mwenendo wa mkutano huo, Jukwaa lilibaini kuwepo kwa kasoro kubwa wakati wa mchakato wa kurejesha uhusiano wa kikazi kati ya vyombo vya habari na kiongozi huyo ambaye habari zake zilizuiwa kuripotiwa kwa takribani miezi mitano” ilisema taarifa ya Jukwaa hilo.

Kikao hicho kiliongozwa na mwenyekiti wa muda, Wallace Maugo ambapo viongozi hao wa TEF walikiri kosa na kuomba radhi kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari bila idhini ya mkutano mkuu wa Jukwaa hilo.

Aidha, wajumbe wa Jukwaa hilo waliutaka uongozi wa TEF kutofanya maamuzi yoyote bila idhini ya mkutano mkuu.

Wiki iliyopita TEF kupitia kwa mwenyekiti wake, Theophil Makunga iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kuondoa zuio la kutomuandika mkuu mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Tangazo hilo la TEF ambalo linadaiwa kutolewa bila kufuata utaratibu wa vikao, limezua mjadala na jana wajumbe wa jukwaa hilo walilazimika kuwapa onyo viongozi waliohusika kufanya hivyo.

Makonda aliingia katika mgogoro na waandishi wa habari mapema mwaka huu, baada ya kudaiwa kuvamia kituo cha Luninga cha Clouds cha jijini Dar es Salaam.

Baada ya tukio hilo waandishi wa habari kupitia TEF walikubaliana kutoandika habari zozote nzuri zinazomhusu Makonda.

error: Content is protected !!