August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahariri, Waandishi wamsusia Makonda

Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Spread the love

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), wameazimia kumnyima Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ushirikiano wa kibahari kwa kutoandika au kutangaza habari zote zinazomhusu, anaandika Pendo Omary.

TEF na DCPC wamechukua hatua hiyo, baada ya Makonda kuvamia kituo cha habari cha Clouds Media, kilichopo Mikocheni, kiasi cha saa 5 usiku, Ijumaa ya wiki iliyopita, akifuatana na polisi wenye silaha na kutaka kulazimisha kurushwa kipindi cha SHILAWADU kwa namna atakavyo.

Taarifa ya asasi hizo za wanahabari imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Theophil Makunga, Mwenyekiti wa TEF, na Jane Mihanji, Mwenyekiti wa DCPC, na kuungwa mkono na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

“Kwa pamoja tumeazimia kutoandika habari zote zinazomhusisha Makonda katika vyombo vyetu vya habari. Kwa mantiki hiyo tunamtangaza Paul Makonda kuwa ni adui wa uhuru wa habari na yeyote yule ambaye anashirikiana au atashirikiana naye katika kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa inasema utekelezaji wa azimio hilo unaanza mara moja kwa vyombo vyote vya habari nchini na utaendelea hadi pale itakapotangazwa au kuagizwa vinginevyo.

error: Content is protected !!