May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahariri Tanzania wampongeza Rais Samia, wampa ujumbe Ndugai na Msigwa

Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile

Spread the love

 

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limempongeza Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, kwa kuagiza vyombo vya habari vyote vilivyofungiwa kufunguliwa. Anaripoti Hamis Mguta (endelea).

Pia, wamemwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kuiga mfano huo, kwa kuruhusu waandishi kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo ya kitaalamu, tofauti na hali ilivyo sasa.

Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema hayo leo Jumanne, tarehe 6 Aprili 2021, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Ni saa chache kupita tangu, Rais Samia kuagiza wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo kuvifungulia vyombo hivyo na kuweka wazi kanuni za adhabu huku akizuia ubabe kutumika kuvifungia.

Baadhi ya magazeti yaliyofungiwa na kunyimwa leseni ni; MwanaHalisi, Mseto, Tanzania Daima, Mawio na televisheni ya mtandaoni ya Kwanza TV.

“Tunampongeza sana, Rais Samia kwa uamuzi mzito na wa kihistoria wa kufungulia vyombo vya habari kama MwanaHalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima ambalo lilifutiwa usajili,” amesema Balile

Amesema, vyombo vya habari, vinafanya kazi nyingi ikiwemo ya kuhabarisha jamii “tunamhakikishia tutafanya kazi kwa weledi kwa mujibu wa taaluma ya habari.”

Balile amesema, kupitia kazi ya vyombo vya habari, vitafungua fursa ajira kwa waandishi wenyewe ambao wamekuwapo mtaani bila kazi kutokana na kadhia ya vyombo vyao kufungwa.

Balile ametumia fursa hiyo, kumwomba Spika Ndugai kuweka mazingira rafiki kwa waandishi kufanya kazi yao wao wenyewe kuliko kusubiri Bunge liwafanyie na kuwapatia, hali ambayo inakwaza utendaji kazi.

Hali ilivyo sasa, Bunge inarekodi kila kitu bungeni kisha inawapatia waandishi maudhui.

Balile anasema “kitendo hicho kinasababisha maudhui mengine kukatwa au kutolewa yasiyokuwa na maana. Spka Ndugai aliangalie hili, sisi tupo pale siyo kuangalia tu kinachoendelea lakini kurekebisha baadhi ya mambo ambayo hayako sawa kwa wabunge.”

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Ametolea mfano, moja ya picha iliyopigwa mbunge akisafisha viatu “picha hii ilileta shida lakini kweli mbunge anaingia bungeni kusafisha kiatu? Kwa hiyo, sisi tuna kazi pia ya kurekebisha tabia.”

Katika hatua nyingine, Balile amemkaribisha, Gerson Msigwa ambaye ameteuliwa na Rais Samia kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kabla ya uteuzi huo, Msigwa alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

“Tunampongeza Msigwa kwa kuteuliwa, amekuwa mwanahabari, tunamkaribisha, amesikia kauli ya Rais Samia, asije kufanya kama yale ya mtangulizi wake,” amesema Balile.

Awali, Dk. Hassan Abbas, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ndiye alikuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.

Gerson Msigwa mkuu wa idara ya habari na maelezo

“Katibu mkuu, Dk Abbas ameona kilichotokea na avae viatu vyetu vya kiuanahabari,” amesema Balile akikumbushia jinsi walivyofanya kazi na Abbas ikiwemo kumtuma kazi mbalimbali akimaanisha maisha ya chumba cha habari anayajua.

Pia, TEF limemwomba Rais Samia kama alivyotoa msimamo kwa wafanyabiashara juu ya ukusanyaji kodi, kufungulia vyombo vya habari “na sisi siyo wanasiasa na hatufurahishwi sana kuona hawafanyi mikutano.”

Amesema, wanapofanya mikutano yao iliyopo kwa mujibu wa Katiba na sheria, itamsaidia Rais Samia na vyombo vingine vya kimamlaka, kuchukua hatua “kwani wamekuwa wakichambua ripoti za CAG na mambo mengine.”

error: Content is protected !!