January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahamiaji watuma mabilioni ya dola kwao

Fedha za kigeni

Spread the love

WAHAMIAJI (Diaspora) ni muhimu kama chanzo cha biashara, teknolojia na ujuzi kwa nchi zao na kwa nchi walizohamia.

Kila mwaka wahamiaji hutuma mabilioni ya fedha kwenye nchi zao za asili kwa ajili ya kusaidia familia zao. Fedha hizo hutumika kununulia chakula, nguo, kugharamia tiba na karo kwa ajili ya watoto.

Kadhalika, fedha hutumika kusaidia shughuli za uzalishaji hasa miradi midogo ya kiuchumi ambayo kwa namna nyingine huchangia katika pato la taifa.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya 2013, inasema takribani Dola 404 bilioni zilitumwa na wahamiaji wanaoishi mataifa mbalimbali Ulaya, Marekani na kwingineko, kwenda nchi zinazoendelea.

Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 3.3 kutoka kilichotumwa mwaka 2012. Ripoti hiyo inasema fedha zilizotumwa dunia nzima na wahamiaji zimekisiwa kufikia Dola 542 bilioni mwaka 2013.

Uhamiaji umekuwa na umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa dunia kwa kuwafanya wafanyakazi wa nchi moja kwenda nchi nyingine na hivyo kuwa wazalishaji zaidi wanaoingiza kipato zaidi tofauti na wanavyokuwa kwenye nchi zao.

Fedha zinazotumwa na wahamiaji zinasaidia kupunguza tatizo la umasikini na hivyo kuongeza nguvu kazi, matumizi makubwa katika elimu na afya, huduma nzuri ya habari hasa kwa kutumia teknolojia, upatikanaji wa huduma za fedha, uimarishaji wa ujasiriamali na biashara, na utayari katika kukabiliana na matatizo kama vile janga la ukame, tetemeko la ardhi, kimbunga, upunguaji wa ajira za watoto.

Benki ya Dunia inasema nchi zinazoongoza kwa kuingiziwa fedha nyingi ni India (Dola 70 bilioni), China (Dola 60 bilioni), Ufilipino (Dola 25 bilioni) na Mexico (Dola 22 bilioni.

Kwa Afrika, Nigeria kupitia raia wake waliopo ughaibuni, ilipokea Dola 21 bilioni mwaka jana, kiwango kilichoongezeka kutoka Dola 10 bilioni za 2010.

Kwa kiwango hicho, Nigeria imekuwa nchi ya tano kupokea fedha nyingi kutoka kundi la nchi zinazoendelea na ya kwanza kwa Afrika.

Zaidi ya wahamiaji milioni 30 wa Kiafrika, sawa na asilimia 3 ya idadi ya Waafrika, wanaishi nje ya nchi zao. Hiyo ni pamoja na kuishi nchi nyingine ndani ya bara la Afrika.

Wakati Watanzania waliopo ughaibuni wakituma kwao Dola 75 milioni, Wakenya mwaka jana tu walituma Dola 1.3 bilioni wakati Uganda ilipokea asilimia 10 zaidi ya kiwango hicho ikiwa ni zaidi mara mbili ya fedha za mauzo ya kahawa nje.

Agosti mwaka huu, fedha za wahamiaji zilizoingia Kenya ziliongezeka kwa asilimia 20.34 ukilinganisha na Agosti 2013. Kwa mujibu wa taarifa za fedha za Benki Kuu ya Kenya (CBK), Dola 128 milioni zilitumwa Kenya mwezi Agosti 2014, kiwango cha juu kulinganisha na Dola 107 milioni zilizotumwa Agosti 2013.

Kuanzia Januari mpaka Agosti mwaka huu, Kenya ilipokea Dola 936 milioni na 2013 ilipokea Dola 1.3 bilioni.

Takwimu hizo zinaonesha kiwango kinachotumwa Tanzania ni kidogo mno mara 17 kulinganisha na Kenya.

Watanzania wanaoishi ughaibuni wanasema sababu zipo nyingi za kutuma kiasi kidogo kulinganisha na jirani zake. Idadi ya wahamiaji wenyewe si kubwa kama wao.

Watanzania walio wengi wanakwepa kutuma fedha kwa njia zinazotambulika kwa kukwepa gharama za utumaji, tofauti na gharama za nchi nyingine kama Nigeria na Kenya.

Gharama zinaonekana pia katika huduma nyingine kama kupiga simu kwani kupiga simu kutoka London kwenda Tanzania ukitumia dola tano inakupa dakika chache kuliko ukipiga Kenya, na ni karibu na bure ukipiga Nigeria au India.

Mkurugenzi wa Wizara aongelea utumaji wa fedha

Kwa mujibu wa Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Tanzania imepitwa na Kenya na Rwanda kwa upokeaji fedha kutoka nje.

Mushy aliwaambia waandishi wa habari wakati wa wiki ya biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, mwezi uliopita, kuwa Kenya na Uganda wamefanya vizuri kwa kuwa na utaratibu mzuri wa utumaji wa fedha.

Utumaji fedha kutoka ughaibuni hukuza uwekezaji katika kukuza nishati, madini, utalii. Hiyo husaidia kuzalisha ajira kwa mamilioni.

Balozi Mushy alipendekeza kutumia Benki ya CRDB akisema ndio ya kwanza iliyofungua akaunti maalumu kuwezesha Watanzania walioko nje kuweka fedha na kufanya miamala.

Ufunguaji wa akaunti utaongeza idadi ya Watanzania wenye akaunti kupitia benki mbalimbali kwani kwa sasa ni asilimia 11 tu yao wanazo akaunti.

error: Content is protected !!