January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wahadhiri wa Kizanzibari wasalimishwa

Spread the love

WATANZANIA sita kutoka Zanzibar, waliotekwa na kundi la waasi nchini Kongo wameachiwa huru baada kundi hilo kudhibitiwa na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Kongo. Anaadika Hamisi Mguta … (endelea).

Watanzania hao walitekwa na waasi wa kundi la Kivu Kaskazini sehemu ya DRC. Wazanzibari hao walikwenda nchi hiyo kwa ziara ya shughuli za kueneza dini ya Kiislam.

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje, Balozi Salim Kombo amesema taarifa walizopata nchini DRC zimesema Watanzania hao wanawakilisha taasisi ya Tabligh.

Bila ya kuwataja kwa majina, amesema hali zao ni salama na kwa sasa wanaishi chini ya uangalizi wa Serikali ya DRC.

Kombo amesema waasi hao walitaka kulipwa Dola 40,000 ili kuwaachia Watanzania hao, kiwango ambacho watekaji walipunguza baada ya kushindikana kupata. Wakataka Dola 20,000.

Balozi Kombo amesema hatimaye wananchi hao waliachiwa bila ya kutolewa fedha yoyote baada ya kufanikiwa kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na DRC.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula amesema taarifa za kuachiwa kwa Watanzania hao zimepatikana usiku wa kuamkia leo kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Kongo, Antony Cheche.

Balozi Mulamula amesema kutekwa kwa Watanzania hao, ni tukio lililotia hofu viongozi kwa sababu ni mara ya kwanza kuwatokea Watanzania kokote kule.

Amesema utaratibu wa kuwahamisha Watanzania kutoka Kivu na kupelekwa mjini Goma unaendelea kufuatiliwa ili wapate kurejeshwa kwao baada ya kukabidhiwa kwa Balozi Cheche aliyetarajiwa kuwasili mjini Goma leo.

Balozi Mulamula amehimiza Watanzania wote wajenge utaratibu wa kufika ofisi za kibalozi za Tanznaia wanaposafiri kwa shughuli mbalimbali ughaibuni. Hiyo inaweza kusaidia kutoa msaada panapotokea dharura. Watanzania hao waliotekwa DRC hawakuripoti rasmi serikalini kuhusu safari yao.

 

error: Content is protected !!