June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wagonjwa wa Covid-19 waongezeka Tanzania

Spread the love

 

WAGONJWA wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid-19), nchini Tanzania, imeongezeka kutoka 408 hadi kufikia 682. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). 

Tarehe 8 Julai 2021, Serikali ya Tanzania ilitoa takwimu za Covid-19, ikisema kwamba kulikuwa na wagonjwa 408, kati yao 284 walikuwa wanapumua kwa msaada wa mashine ya oksijeni.

Leo tarehe 22 Julai 2021, Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, amesema hadi kufikia jana idadi ya wagonjwa waliolazwa katika vituo vya afya ni 682.

“….. kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa waliolazwa, ambapo kufikia tarehe 21 Julai 2021, katika vituo vya huduma za afya kote nchini kulikuwa na wagonjwa 682, waliokuwa wanaugua maradhi ya Covid-19,” amesema Dk. Gwajima.

Waziri huyo wa afya amesema, ongezeko hilo limesababishwa na mwitikio mdogo wa wananchi, katika kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Serikali inatambua kuwa, wananchi walio wengi wamekuwa wasikivu, wakiitikia na kutekeleza miongozo yote ya kujikinga na kuwakinga wengine, ingawa kwenye baadhi ya maeneo mwitikio umekuwa siyo wa kuridhisha. Hali hii imeendelea kuchangia kuongezeka kwa maambukizi,” amesema Dk. Gwajima.

Kufuatia ongezeko hilo, Dk. Gwajima ametoa wito kwa watanzania kufuata miongozo ya kushibiti maambukizi ya Covid-19.

“Wito wangu tuendelee kushikamana kwenye mapambano ya kutokomeza kabisa adui Covid-19, kwa kuzingatia utekelezaji wa afua zote za kujikinga na kuwakinga wengine zikiwemo, kuhakikisha sehemu zote zinazotoa huduma za kijamii zinakuwa na miundombinu ya huduma ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kama maji hakuna kuwe na matumizi ya vitakasa mikono,” amesema Dk. Gwajima na kuongeza:

“Wananchi wote wanaotoa huduma za kijamii na wanaofika kupata huduma za kijamii wahakikishe wamezingatia afua za kinga, zikiwemo kuvaa barakoa safi na salama na mwenye maeneo ya huduma za kijamii zinazokutanisha watu  kupata huduma ,kanuni ya kuepuka misongamano izingatiwe kwa kuchukua tahadhari zote.”

error: Content is protected !!