September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wagonjwa wa Corona Tanzania waongezeka

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imetangaza wagonjwa wanne wapya wa Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akitangaza taarifa ya wagonjwa hao leo tarehe 6 Aprili 2020, Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya amesema wagonjwa hao wanaifanya Tanzania kuwa na wagonjwa 24.

Katika taarifa yake kwa umma, Waziri Ummy amesema kesi hizo mpya nne, zimepatikana jijini Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.

“Wizara inathibitisha kuwepo kwa kesi mpya nne za maambukizi ya COVID-19 zilizopatikana Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar, na kufanya kuwepo kwa jumla ya kesi 24 zilizoripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini,” inaeleza taarifa ya Waziri Ummy.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, wagonjwa wawili kati ya wanne waliotangazwa leo, taarifa zao zilitolewa tarehe 5 Aprili mwaka huu na waziri wa afya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wagonjwa wawili wa Tanzania Bara ni, mwanaume (41) mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza aliyeingia nchini akitokea Dubai, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuelekea Mwanza tarehe 29 Machi 2020.

Mwingine ni mwanaume (35) raia wa Tanzania, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.

“Wagonjwa wote wako chini ya uangalizi wa watoa huduma za afya katika vituo maalumu vya tiba Dar es Salaam, Zanzibar na Mwanza. Wizara ya afya inaendelea kuwafuatilia waliowahi kukutana na watu hao ili kudhibiti maambukizi mapya,” inaeleza taarifa ya Waziri Ummy.

error: Content is protected !!