January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wagombea ubunge, uwakilishi CUF hawa

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza majina ya wanachama wake watakaogombea viti katika Bunge na Baraza la Wawakilishi na kuridhia maamuzi yaliyofanywa majimboni na wananchi. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Umma, wanachama wapya waliojiunga wakitoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuomba uteuzi wamepitishwa.

Hawa ni pamoja na Juma Hamad Omar, mwanasiasa aliyefikia ngazi ya waziri katika Serikali ya Muungano, akihudumu sekta ya Maliasili na Utalii.

Hamad ambaye aliteuliwa nafasi hiyo wakati wa uongozi wa Ali Hassan Mwinyi, ameteuliwa kugombea ubunge jimbo la Ole wakati Ahmed Juma Ngwali aliyekuwa mbunge Ziwani, ameteuliwa kugombea Wawi, jimbo alilokuwa akiwakilisha Hamad Rashid Mohamed, ambaye baada ya kufukuzwa uanachama 2012, amejiunga na Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) na ameteuliwa kugombea urais wa Zanzibar. ADC kiliundwa mwaka 2013 na waliokuwa makada wa CUF, yeye Hamad akiwa Mlezi wao.

Katika uteuzi huo, CUF imeshikilia uamuzi wa wananchi wa majimbo ya Mkanyageni na Gando ambako wabunge wake mashuhuri, Mohamed Habib Mnyaa, na Khalifa Suleiman Khalifa, wametupwa kwenye kura za maoni.

Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein ambaye aliingia bungeni mwishoni mwa mwaka jana kupitia uchaguzi mdogo, ameteuliwa kutetea kiti hicho. Yussuf pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama.

Wengine mashuhuri walioteuliwa kutetea viti ni Khatib Said Haji (Konde), Haji Khatib Kai (Micheweni), Rashid Ali Abdalla (Tumbe), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando).

Kwa upande wa uwakilishi, chama kimewateua wanachama waliohama CCM akiwemo Mansour Yussuf Himid anayegombea jimbo la Kiembesamaki, alikokuwa mwakilishi akiwa CCM.

Mwanasiasa kijana aliyepata umaarufu haraka kwa kutetea hoja ya kuwa na Muungano wa haki wa serikali tatu, anaongoza timu inayosimamia mkakati wa kumpatia ushindi Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad, mgombea tena urais. Maalim Seif pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kada mpya mwingine ni Mohamed Hashim Ismail, naibu waziri mstaafu serikalini aliyeteuliwa kugombea uwakilishi jimbo la kwao Dimani, Wilaya ya Magharibi, Unguja.

Hashim ni swahiba mkubwa wa Amani Abeid Karume, rais mstaafu wa Zanzibar ambaye pamoja na Maalim Seif walifanikisha kufikiwa kwa muafaka wa kufuta siasa chafu na kuanzisha siasa za maridhiano zilizowezesha kufanywa mabadiliko ya katiba na kuundwa serikali ya umoja ya vyama vilivyo hasimu vya CCM na CUF.

Mwanasheria mashuhuri Iss-hak Ismail Shariff ameteuliwa kugombea uwakilishi jimbo la Wete, sambamba na wawakilishi wazoefu Said Ali Mbarouk (Gando), Omar Ali Shehe (Chake Chake), Hija Hassan Hija (Kiwani) na Ismail Jussa Ladhu (Malindi).

Katika uchaguzi ambao kura itapigwa Oktoba 25, Wazanzibari watachagua Rais wa Zanzibar, mwakilishi na diwani unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), pamoja na Rais wa Muungano na mbunge unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Hata hivyo, kwa ubunge watapiga kura majimbo 50, pungufu ya manne yaliyoongezwa kwa upande wa uwakilishi.

Uchaguzi umepata uchangamfu zaidi kutokana na CUF kuongeza nguvu ya mkakati wa ushindi baada ya kushirikiana na Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) uliomkaribisha kada wa enzi kutoka CCM, Edward Lowassa na kumteua kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chadema.

error: Content is protected !!