Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ubunge, udiwani CCM kaa la moto, Takukuru, Polisi wapewa rungu
Habari za SiasaTangulizi

Ubunge, udiwani CCM kaa la moto, Takukuru, Polisi wapewa rungu

Humphrey Polepole, Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM
Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, kimetoa utaratibu mpya utakaotumika kuwapata wagombea udiwani, ubunge na uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, chama hicho, kimezitaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) na Jeshi la Polisi kuwasana na kuwashughulikia wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa maadili ya chama kabla ya wakati.

Hayo, yamebainishwa leo Jumanne tarehe 2 Juni 2020 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Polepole amesema, mchakato wa kuwapata wagombea ubunge na uwakilishi utaanza baada ya Bunge na Baraza la Wawakilishi kuvunjwa kwa mujibu wa sheria kisha, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza ratiba.

“…wakati huo tu ndipo wana-CCM ambao kwa unyenyekevu mkubwa, wanaomba dhamana kugombea kupitia CCM watapa fursa,” amesema Polepole.

“Kipindi cha sasa, bado wapo kwenye uongozi wabunge, wawakilishi na udiwani na wakati huu ambapo bado wanawatumikia wananchi, tuwape muda wamalize muda wao,” amesema.

Polepole amesisitiza, “sote tusubiri utaratibu wa chama ili kuondoa mvurugano, migongano isiyokuwa ya lazima na tija inayodhoofisha umoja wa chama chetu.”

Amesema, mchakato wa kupata mgombea wa CCM ndiyo mchakato bora kwa nchi zote Afrika zenye mlengo sawa na wao.

Polepole amesema, mchakato utakaotumika mwaka huu, unatofauti kidogo na ule wa mwaka 2015.

Amesema, mwaka 2015, mgombea ubunge alitakiwa kupita kata kwa kata ili kupigiwa kura za maoni “na tathimini tuliyoifanya, ulikuwa na uvunjifu na mapungufu kwa maana ya kuacha mianya” na ndiyo maana wameamua kuubadili na kuanzisha mpya kwa maslahi ya chama na nchi kwa ujumla.

Akiuelezea kwa kina utaratibu huo, Polepole amesema, baada ya kuwatangazia mchakato kuanza, mwana-CCM anayetaka kugombea hatoruhusiwa kwenda kuchukua fomu kwa mbwembwe ikiwemo matarumbeta.

Amesema, mwanachama atakwenda ofisi za chama hicho wilaya, “kwa unyenyekevu mkubwa siyo kwa tarumbeta, hizo tarutemba utakuja tukishakuwa na mgombea mmoja.”

Polepole amesema, baada ya fomu kuchukuliwa na wanachama kwa idadi yoyote ile, vikao kwa ngazi ya wilaya vitafanyika kujadili huku upande wa Zanzibar kikao cha kamati ya siasa ya halmashauri ngazi ya jimbo vitajadili, “ana sifa, mwana-CCM mzuri au huyu mtu ana tabia ya ulevi kwa kweli anakiabisha chama.”

Amesema, kamati ya siasa ya wilaya, mkoa na sekretarieti ya halmashauri kuu kitawajadili kwa nafasi zao na kutoa mapendekezo kisha kamati kuu itakawajadili na kisha kuteua majina matatu, “ambayo majina hayo yatakuwa ni siri kubwa na kuwekwa muhuri wa moto.”

“Kisha majina yatarejeshwa katika mikutano ya jimbo ya ubunge na uwakilishi” ambapo kikao cha jimbo kina wajumbe kati ya 800 hadi 1,000.

Polepole amesema, “bahasha ile itakuja, itafunguliwa ambapo kwa mara ya kwanza majina matatu yaliyopata uteuzi kutoka kamati kuu, baada ya kujiridhisha pasina shaka kwamba watu hawa hawana tashwishwi.”

Amesema, baada ya kupigwa kura, zitaonyesha nani amepata kura ngapi hadi wa tatu na, “mchakato huo, utatengenezewa muhtasari, zile taarifa zitakuja makao makuu ya CCM Taifa.”

Polepole amesema, mchakato wa kujadili na kutoa mapendekezo kwa majina hayo matatu kwa mara ya pili  tena, kamati ya siasa jimbo kwa Zanzibar, kamati ya siasa ya wilaya kwa bara.

“Kisha kamati ya siasa ya mkoa itajadili na kutoa mapendekezo, sekretarieti ya  Halmsahauri Kuu ya Taifa (NEC) na kutoa mapendekezo, kamati kuu itajadili na kutoa mapendekezo kisha halmashauri kuu ya taifa itajadili na kuteua jina moja,” amesema

Polepole amesema, jina hilo moja sasa ndilo litapelekwa NEC kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge na uwakilishi.

Akigusia mchakato wa udiwani, Polepole amesema mchakato utakuwa kama huo wa ubunge na uwakilishi kwa fomu kuchukuliwa ofisi za kata, kasha vikao vitakavyofanyika kujadili majina ni vya kata, wilaya kisha mkoa.

Amesema, mkoa utapendekeza majina matatu yakakayorudishwa kwenye mkutano mkuu wa kata ambao utapiga kura za maoni na majina yatapelekwa ngazi ya mkoa huku vikao vya kujadili majina hayo kwa ngazi ya kata na wilaya vikifanyika ikiwamo kutoa mapendekezo.

“Ule mchakato wa mwanzo, tulikuwa tunatumia kadi za ujanja ujanja. Utaratibu wa sasa, tutatumia kielektroniki, yaani mjumbe anatoa kitambulisho chake, anaingia ndani na atakayekuja kama mamuruki mtaumbuka na tunataka haki itamalaki,” amesema.

“Utambulisho huu, utafanyika kwa vikao vyote Jimbo na wilaya na Mkutano Mkuu wa Taifa kwani utaratibu unakwenda vizuri na jana Mwenyekiti wetu, John Magufuli alikagua ukumbi wa mikutano,” amesema.

Polepole amesema, “umuhimu wa nidhamu ya chama na usimamizi wa maadili. Tunaposimamia haki na maadili ya viongozi, tunaweza kupata wagombea wanaopatikana kwa matakwa ya wananchi na Watanzania na kukiacha chama kikiwa salama.”

Kuhusu mikakati yake ya kukabiliana na rushwa, Polepole amesema, “rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa. Hii itoshe kufahamu kwamba, katika uchaguzi huu, rushwa haina nafasi na kauli imekwisha kutolewa, chama kitawasaka, kutafuta wote wanaosaka uongozi kwa kutumia rushwa.”

“Iwapo katika mkoa au wilaya, Bara na Zanzibar kwamba viongozi waliojihusisha na vitendo vya rushwa na kuwanyima viongozi, harafu taasisi zinazohusika na rushwa hazitachukua hatua, chama hakitaona ajizi kuelekeza serikali kuwachukuliwa hatua viongozi wa taasisi hizi,” amesema.

Polepole ametumia fursa hiyo, kupiga marufuku watu kufanya vitendo vinavyohusiana na kuanza kampeni mapema kama kutoa misaada, kujitambulisha au kwa namna yoyote ile, watachukuliwa hatua ikiwemo kunyimwa dhamana ya kugombea.

“Wako watu wanajipitisha mikoani na majimboni kwa kisingizio cha kuchangisha fomu za urais, sisi wana CCM tunajua kwamba kwa desturi yetu mgombea urais anajulikana. Polisi, Takukuru kamateni hao kwa matumizi mabaya ya michango hiyo,” amesema Polepole.

“Wako kundi lingine, wanajiita watafiti wa chama, eti wanatafiti kukubalika kwa wabunge, hawa nao wachukulieni hatua na tunao watu waliokwisha kufanya kazi hiyo na wanaojipitisha huko, kuwapuuza watu hawa,” amesema.

Pia, Polepole ametangaza namba mbili zitakazotumika kupokea taarifa mbalimbali zinazohusiana na vitendo vya rushwa ili kuwachukulia hatua wahusika wote.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!