January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauaji ya Albino, waganga, wapiga ramli wapigwa marufuku

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari, kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzania, Ernest Kimanya

Spread the love

WAGANGA wapiga ramli, wamepigwa marufuku kufanya shughuli zao nchini. Marufuku hiyo imekuja baada ya uchunguzi kubaini, wanahusika na mauaji ya walemavu wa ngozi (albino), anaripoti Sarafina Lidwino.

Marufuku hiyo imetolewa na serikali ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ametangaza leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofsini kwake.

Chikawe amesema, uchunguzi uliofanywa na  Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Maalbino Tanzania, kuanzia mwaka 2006 hadi sasa, unaonesha waganga hao ndio wamekuwa chanzo cha kutokoma kwa mauaji hayo. Wamekuwa wakitumia ramli kuwaagiza watu kutumia viungo vya albino kujipatia utajili.

“Mkakati wa kuwasaka waganga wapiga ramli utaaza baada ya wiki mbili na tumepanga kuweka jitihada katika mikoa ya Mara, Mbeya , Tabora, Mwanza na Shinyanga kwa sababu ndiyo inayoongoza kwa matukio haya, huku pia wapiga ramli wakiwa wengi  zaidi,” amesema Chikawe.

Chikawe amebainisha kuwa, “tutatembea mtaa kwa mtaa kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa kuwasaka wapiga ramli. Watanzania tunatakiwa kujua kuwa, hawa pia ni watanzania wenzetu na wana haki kama sisi. Tofauti  yetu ni rangi ya ngozi hivyo hakuna sababu ya kuwabagua.”

Kuhusu kutoweka kwa mtoto Pendo Emmanuel (4), mkazi wa kijiji cha Ndami, Tarafa ya Mwamashimba, Wilaya ya Kwimba, Mwanza aliyetoweka saa 4:30, 27 Disemba, 2013 baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba yao kisha kumbeba kwa nguvu Chikawe amesema “tayari watuhumiwa 15 wamekamatwa”

Hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya albino nchini Chikawe amesema, hukumu nyingi zimechelewa kutolewa kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha. Licha ya changamoto hiyo serikali itahakikisha ushahidi usio na shaka unapatikana.

 “Wananchi wote wanahusika katika jambo hili. Tunaomba ushirikiano wenu.  Viongozi wa kidini wote ombeni   juu ya hili suala, mnapokuwa na waumini wenu muwaambie juu ya dhambi hii, kuwa si nzuri. Kwa sababu hawa pia ni viumbe wa Mungu,” amesema Chikawe.

Aidha amesema, serikali imejipanga kupambana na watu wote wanaohusika na mauaji au manyanyaso yoyote yanayohusiana na albino. Katika kufanikisha hilo tayari kuna timu ya watu wapo sehemu mbalimbali nchini kuchunguza wahusika wa mauaji hayo.

error: Content is protected !!