January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waganga 1600 wabainika kutosajiliwa

Sehemu ya vifaa vya waganga wapiga ramli

Spread the love

ZAIDI ya waganga 1600 wa tiba asilia katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamengundulika hawajasajiliwa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambapo mpaka sasa ni 164 pekee waliosajiliwa. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Hayo yamebainishwa juzi mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, wakati wa mkutano uliowahusisha waganga wa tiba asilia na watumishi wa ngazi tofauti kutoka serikalini.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Henry Nyamete, amesema idadi hiyo ya wanganga imengudulika baada ya sensa iliyohusisha Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo.

“Wanganga walio wengi wanapiga ramli chonganishi kinyume na sheria, pia wanatoa huduma huku wakiwa hawajasajiliwa na hatutakubali kuona kitendo hicho kinaendelea kufanyika,” amesema Nyamete.

Nyamete pia amesema waganga wa tiba asilia nchini wanapaswa kujisajili ili waweze kufanya kazi zao kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo, aliwataka waganga na watazania kwa ujumla kuhakikisha wanaachana na imani potofu ya kuwauwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) na vikongwe kwa kuwakata viungo vyao.

Mkumbo amesema vitendo hivyo vinatokana na imani potofu iliyojengeka kwa baadhi ya watu kwamba kumkata Albino ama kikongwe kiungo chake watapata utajiri, kitendo ambacho kinalitia doa taifa.

“Hata mauaji yanayotokea katika migogoro ya ardhi yanatotokana na upigaji ramli chonganishi na sasa yameshamili sana nchini, tunapaswa kupinga mambo ya namna hii kuendelea kutokea,” amesema Mkumbo.

Naye Afisa Misitu Wilaya ya Sengerema, Paulo Pontian, amesema baadhi ya waganga wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kufuata sheria huku wakitumia nyaraka za Serikali, akitolea mfano, pembe ya swala kuwa faini yake ni dola 200 au kufungwa gerezani miaka 10.

error: Content is protected !!