August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafugaji waomba afueni kwa serikali

Ng'ombe wakiwa machungoni

Spread the love

WANACHAMA wa Chama cha Wafugaji Tanzania, wilayani Kilombero, Morogoro wameiomba serikali kuweka utaratibu utakaowawezesha kuondokana na vipigo, manyanyaso na maafa wanayoyapata kutoka kwenye hifadhi zilizopo jirani na maeneo yao, anaandika Christina Haule.

Ombi hilo lilitolewa leo na mmoja wa wafugaji hao, Mpenda Chai kwenye mkutano wa chama cha wafugaji hao na uongozi wa wilaya hiyo ukiongozwa na James Ihunyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero.

Mkutano huo umefanyika kwenye Kijiji cha Kyela, Kata ya Chita Tarafa ya Mlimba wilayani Kilombero.
“Utakuta wakati mwingine ng’ombe, kaingia tu hifadhini sababu mnyama hajui lolote, au katika kuchunga ukajisahau ukaingia hifadhini, wahifadhi wakikukuta, kama sio kutoonekena kabisa basi utarudi na majeraha,” amesema Chai.

James Ihunyo, Mkuu wa Wilaya hiyo amekemea tabia ya wahifadhi kujichukulia sheria mikononi ambapo amewataka jamii kutoa taarifa mapema inapofanyiwa ukatili huo atakayehusika kufanya unyanyasaji huo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Amesema, ni vyema wananchi wakajenga utaratibu wa kutoa taarifa mapema kwenye vyombo vya dola na kwamba, akiwa kama mkuu wa wilaya hatokubali kuendelea kuona wananchi wananyanyanswa.

“Kisheria mtu akiingia hifadhini hapaswi kupigwa wala kufanyiwa ukatili wowote, atakayepigwa atoe taarifa polisi na mhusika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria” amesema.

Ndonya Sagumbi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani Kilombero, ameitaka serikali kuona umuhimu wa kuwajengea marambo ya kunyweshea mifugo yao kufuatia kukosa maji katika maeneo yao.

Sagumbi amesema, wanafikwa na wakati mgumu kwa kukosa maeneo ya kunywesha mifugo yao na kufikia wanyama kupungua uzito na kukosa soko la uhakika kwenye minada.

Mustafa Makuka, Ofisa Mifugo Msaidizi wa wilaya hiyo aliwataka wafugaji kuacha tabia ya kupokea wageni na kuwahifadhi kwenye maeneo yao kwani kufanya hivyo kunafanya idadi ya mifugo kuongezeka na kutoendana na usawa wa eneo lililopo.

Makuka amesema, wilaya hiyo haina eneo la ziada lililotengwa kwa ajili ya wafugaji bali eneo lililopo litumike kwa idadi ya mifugo inayotakiwa na mifugo itakayozidi iuzwe kwa kufanya shughuli zingine za kuleta manufaa na maendeleo kwa ujumla.

Amefafanua kuwa, kata hiyo ya Chita ina vijiji vitatu kikiwemo Melela chenye eneo la hekta 713.3 lililotengwa kwa ajili ya kutosheleza ufugaji wa ng’ombe 891, Idunda chenye hekta 145.3 eneo lenye uwezo wa kutosheleza ufugaji wa ng’ombe 181 na Msita lenye hekta 1114.3 lenye uwezo wa kutosheleza ufugaji wa ng’ombe wasiozidi 1392.

 

error: Content is protected !!