September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wafugaji wamfikishia kilio Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

WAFUGAJI nchini Tanzania, wameioomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, itatue changamoto zinazowakabili, ikiwemo mifugo yao kushikiliwa na hifadhi ya wanyamapori kinyume cha sheria. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Jumanne, tarehe 7 Septemba 2021 na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura, kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya mifugo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jijini Dar es Salaam.

Wambura amemuomba Waziri Majaliwa afikishe kilio chao kwa Rais Samia, huku akisema ng’ombe zaidi ya 5,000 zinashikiliwa katika hifadhi mbalimbali, licha ya wamiliki wake kushinda kesi katika migogoro iliyopelekea mifugo hiyo kushikiliwa.

“Kabla sijatoa salamu nikuombe upokee salamu za wafugaji na zimfikie Rais Samia, waziri mkuu katika hifadhi mbalimbali ziko ng’ombe zaidi ya 5,000 zinashikiliwa hatuwezi kupata maziwa wakati ng’ombe wanashikiliwa, ndama wanaachwa nyumbani wanakufa sekta hii haiwezi kuwa salama,” amesema Wambura.

Wambura amesema “zipo kesi wafugaji wameshinda lakini mpaka sasa hawajapewa mifugo yao, wafugaji walioko hifadhi ya Burigi wameshinda kesi, mhifadhi ameng’ang’ania ng’ombe na maeneo mengine, kwa kuwa umefika Waziri Majaliwa tunaamini itakwenda kuachiwa.”

Aidha, mwenyekiti huyo wa wafugaji Tanzania, ameiomba Serikali isimamie zoezi la utambuzi wa mifugo, ili kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa haki za wanyama.

“Tunalo zoezi la utambuzi wa mifugo kwa hereni, tuombe namna bora kupitia kamati ya operesheni ya mifugo ifanywe kwa weledi, lakini isifanywe kabla ya kumshirikisha waziri wa mifugo. Kwa sababu kwenye operesheni hizi sheria ya haki za wanyama zinakiukwa,” amesema Wambura.

error: Content is protected !!