January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafugaji waigaragaza KADCO

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akihutubia mkutano wa hadhara huko Meru

Spread the love

KATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ameonja joto ya jiwe. Wiki mbili zilizopita, alipokelewa kwa maandamano makubwa na halaiki na wananchi wa kabila la Maasai kutoka vijiji vinane vya wilaya za Hai na Meru vinavyopakana na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).

Walimweleza jinsi KADCO (Kilimanjaro Airports Development Company) inavyotishia kuwapora ardhi yao ya urithi yenye ukubwa wa karibu hekta 11,448, ambao ni mkubwa kuliko jiji la Arusha.

Katika sakata hili, watu zaidi ya 20,000 wataathirika moja kwa moja; mifugo zaidi ya 100,000, shule 18 za serikali, zahanati, nyumba za ibada – makanisa na misikiti – pamoja na miundo mbinu iliyomo.

Kutoka mwaka 1989 wafugaji hawa wamekuwa wakikabiliana na zahma ya kila aina pamoja na vitisho vya kunyang’anywa ardhi yao ya urithi kwa kizingizio cha upanuzi wa KIA.

Kati ya mwaka 2000 na 2011, Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alifikisha mgogoro huo katika Bunge na kujibiwa hovyo hovyo na serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alikwenda katika vijiji hivyo na kutoa matamshi ya kibabe na kejeli dhidi ya wafugaji na wakulima. Alisema, “ni lazima mtahama kutoka ardhi ya KIA.” Walifugaji walikasirika kupita kiasi. Maelfu kwa maelfu wakaandamana tarehe 27 Machi 2014 kulaani ubabe na uzandiki huo wa KADCO na Gama.

Walienda hadi Dodoma kwa nia ya kumwona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Badala yake walikutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa niaba ya waziri mkuu. Inasemekana Lukuvi alimpigia simu Gama na kumwonya juu ya vitisho hivyo na kumtahadharisha asijaribu kuwaondoa wafugaji.

Lukuvi pia aliwakutanisha wafugaji hao na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe. Mwakyembe aliunda kamati ya watu 15 na kuiagiza itatue mgogoro huo haraka. Hii ilikuwa 28 Mei 2014.

Lakini sasa, ni karibu mwaka mzima kamati hiyo bado haijatatua mgogoro huo.

Lakini Maasai wamevamia KIA? Siyo kweli. Maasai walikuwepo katika mbuga wanayoiita Sikirari toka enzi na enzi. Serikali ya Rais Julius Kambarage Nyerere, ilionyesha nia ya kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa katika ardhi ya wafugaji. Wafugaji hawakukubali.

Mwalimu Nyerere alilazimika kwenda Monduli kuonana na kiongozi wa kiroho wa Maasai (Oloiboni), Ndoros Mbatiany. Nyerere na Mbatiany wakawashawishi Maasai kukubali uwanja wa ndege ujengwe katika eneo lenye ukubwa wa hekta 460 tu, yaani eneo la sasa lenye uzio.

Wafugaji hawakulipwa fidia wala kupewa ardhi mbadala kwa mujibu wa Sheria ya Unyakuaji Ardhi Namba 7 ya 1947. Serikali ya Italia iliipa Serikali ya Tanzania mkopo wa Sh. 100 milioni. Fedha hizi zilitumika kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Ujenzi wa KIA ulianza Mei 1969. Nyerere aliufungua rasmi uwanja huo tarehe 2 Desemba 1971.

Kutokana na kelele za kutisha za ndege hasa nyakati za usiku, familia nyingi zaidi zililazimika kukimbia na kuhamia umbali wa kilometa tatu au zaidi kutoka kwenye uzio wa uwanja.

Ndio maana leo kuna eneo linaonekana kama vile liko wazi lisilo na makazi ya watu pembezoni mwa uzio wa uwanja. Hili ni eneo muhimu sana la malisho! Wanaoitwa wawekezaji wanamezea mate ardhi hii.

Wizara ya Ardhi, bila kuvishirikisha vijiji, ilitenga kilomita za mraba 110 kwa kisingizio cha kuendeleza Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro. Mkutano wa pamoja wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro uliofanyika tarehe 1 Agosti 1985 ulioidhinisha mpango huo bila kufuata maelekezo ya Sheria ya Unyakuaji Ardhi Namba 47 ya 1967.

Mwaka 1986 KIA ilipima eneo hili. Wizara ya Ardhi kimya kimya na kwa usiri mkubwa iliipa KIA hati Namba 23164 mwaka 1989.

KADCO ilianzishwa tarehe 1 Machi 1998 na ilisajiliwa kwa namba 33616. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa na hisa asilimia 24, Mott McDonald International ya Uingereza yenye asilimia 41.4 ya hisa, Inter Consult Ltd ya Tanzania hisa asilimia 44.6 na South African Infrastructure Fund yenye asilimia 30 ya hisa kwa mujibu wa taarifa maalum za kumbukumbu za Bunge – Hansard ya 10 Novemba 2003.

Ukijumlisha asilimia ya hisa hizo unapata 140%. Ni dhahiri Serikali ilikuwa inampiga changa la macho Mbunge wa Hai aliyeuliza KADCO ni nani kwa niamba ya vijiji hivi.

Mkataba wa hiari wa miaka 25 kati ya Serikali ya Tanzania na KADCO ulisainiwa tarehe 17 Julai 1998. Tarehe 4 Agosti 2011 Waziri wa Uchukuzi alimjibu tena Mbowe bungeni kuwa eti Serikali ilivunja mkataba huo batili kati yake na KADCO baada ya kugundua vipengele 47 kati ya 49 vyenye utata; yaani ufisadi kwa Kiswahili. KADCO ni mradi mkubwa wa mafisadi!

Pamoja na mapungufu haya ya kisiasa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi, na bila kuzingatia kuwa mgogoro huu ulifika hadi bungeni mara kadhaa kati ya mwaka 2000 na 2006, KIA ilipewa cheti cha ardhi Namba 22270 tarehe 20 Aprili 2006 kwa miaka 99.

Vijiji hivi vilisajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vijiji vya Ujamaa Namba 21 ya 1975. Msajili wa Vijiji naye alivisajili vijiji hivi kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7 ya 1982. Na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya 1999 inalinda kikamilifu ardhi ya vijiji hivi.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro haujaweza kutumia ipasavyo eneo la hekta 460 zilizoko ndani ya uzio (ambazo Maasai hatukulipwa fidia wala kupewa ardhi mbadala zilipochukuliwa). KIA haihitaji hekta 11,000 kama KADCO inavyodai.

Uwanja wa ndege mkubwa kuliko yote duniani ni Uwanja wa Ndege wa Hartsfield-Jackson Marekeni wenye ukubwa wa hekta 1,902 tu. Mwaka 2013 ndege 900,000 zilipita uwanja huo zikiwa na abiria milioni 94 pamoja na tani 600,000 za mizigo.

Mwaka huo, 2013 KIA ilipitisha ndege 21,791 zikiwa na abiria wasiofika hata milioni moja pamoja na tani 3,500 za mizigo. KIA itahitaji miaka 200 kuufikia Hartsfield-Jackson.

Kinana aliahidi kufikisha kilio hiki kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Je, Kikwete atachukua hatua gani? Ataliweza? Au naye ameshamezwa na wawekezaji?

Makala hii imeandikwa na Navaya ole Ndaskoi 0754453192

error: Content is protected !!