WAFUGAJI wa Nyuki nchini wameshauriwa kutumia zana za kisasa katika ufugaji wa nyuki na kuandaa asali ili kupata bidhaa yenye ubora. Anaripoti Selemani Msuya, Mbeya… (endelea)
Ushauri huo umetolewa na Mtaalam wa Ufugaji Nyuki kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi veta Dakawa mkoani Morogoro Theodora Kiyungu wakati akizungumza na mwandishi wa Mwanahalisi Online, alipotembelea banda la VETA lililopo katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Kiyungu amesema wafugaji wengi wa nyuki nchini wanatumia mbinu za kizamani katika ufugaji na uchakataji wa asali hali ambayo inasababisha thamani ya bidhaa hiyo kushuka.
Mtaalam huyo alisema wapo wafugaji wa nyuki ambao wanachakata asali kwa kutumia chandarua hali ambayo ni hatari kwa afya ya watumiaji.
Amesema VETA Dakawa wanatoa mafunzo ya namna ya kufuga nyuki na kuchakata asali ambayo inakubalika katika soko la ndani na nje.
Pia alisema wanatumia bomba la kisasa kwa ajili ya kutoa moshi na kuwataka wafugaji kuacha kutumia kuni kama njia ya kufukuza nyuki ili kuvuna asali.
“Zao la asali ni moja ya zao muhimu na linalotumika duniani kote, hivyo ni lazima utaratibu wa ufugaji na uchakataji uwe wa kisasa na unaofaa kwa matumizi ya binadamu. Sisi tunaamini wafugaji wakija VETA Dakawa watapata mafunzo sahihi,” alisema.
Alisema pamoja na kupata asali ambayo inatumika kwa jamii, pia kupitia asali wanaweza kupata nta kwa ajili ya utengenezaji wa mishumaa na bidhaa nyingine.
Leave a comment