February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wafugaji: Kupiga chapa mifugo mwarobaini wa mgogoro

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Thomas Silomi, akiwa anazungumza na wakazi wa Loliondo, kuhusu mikakati ya kudhibiti mifugo yao isiweze kuingia kwenye pori tengefu la Loliondo

Spread the love

BAADA ya kudumu kwa mgogoro wa Ardhi kwa muda mrefu katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha kati ya wafugaji na hifadhi, jamii ya Wafugaji wa eneo hilo, wamesema wanatamani zoezi la upigaji chapa mifugo lianze hata leo, anaandika Nasra Abdallah.

Mwenyekiti Wa Wilaya ya Ngorongoro, Thomas Siloma amesema hayo, wakati wa mkutano na wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Loliondo, ambao walianza kuondolewa kwa nguvu kwa kuchomewa maboma yao na kukamatwa kwa mifugo kwa kile kilichodaiwa wamevamia hifadhi hiyo wakati sio kweli.

Siloma amesema wakati wa operesheni hiyo walipachikwa majina mengi, ikiwemo kuitwa wakenya wakati wao ni watanzania waliozaliwa na kukulia hapohapo.

“Kwa nyakati tofauti tumewasikia mawiziri wa mifugo wakisema kutaanza zoezi la kupigwa chapa mifugo ili kuitambua na kuitenganisha na ile ya nchi za jirani hususani Kenya ambao tunaingiliana kwa kiasi kikubwa kimipaka.

“Zoezi hili tungependa lianze haraka sana hata leo ili kutuepusha na dhambi ya kuitwa wakenya na baadhi ya watu wasitutakia mema na Ardhi yetu hii,” amesema Siloma.

Naye Maiko Peliani amesema ili kuepusha migogoro isitokee tena, ipo haja ya maamuzi yanayotolewa na viongozi ikiwemo ya Waziri wa Maliasili wa sasa, Dk. Hamis Kigwangalla, kuwekwa katika maandishi badala ya kubaki kuwa matamko ya mdomoni.

Peliani amesema tatizo hilo la kutowekwa kwenye maandishi matamko ya viongozi limekuwa sababu ya wananchi kuendelea kunyanyaswa na baadhi ya watendaji kwa kisingizio hawajaambiwa na mkuu wao wa kazi.

Kwa upande wake Thomas Kairuu amesema hivi sasa hawatakuwa tayari kuwavumilia watu wanaoswaga mifugo yao kwa makusudi na kuiingiza kwenye hifadhi ili wao waonekane wakosaji kumbe sivyo.

Kairuu amesema tangu waziri asitishe operesheni ya kuondoa wafugaji, kumekuwa na hujuma zinafanywa juu yake yakuonesha kwamba zuio lake hilo limesababisha sasa wafugaji kuingiza mifugo hifadhini wanavyotaka wakati siyo kweli.

“Tunaadhimia katika mkutano huu,yoyote tutakayembaini kutufitinisha na serikali kwa kuingiza mifugo kwa lazma ili wapate picha na habari za kupika kwamba tumekiuka maagizo ya waziri tutakula naye sahani moja kwa kuwa hawa ndio wasiotaka mgogoro huu wa ardhi uishe ili tuweze kukaa na sisi kwa amani kama watu wengine aa nchi hii,” amesema mwananchi huyo.

error: Content is protected !!