August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafuasi wa Lipumba, CUF ngoma nzito

Spread the love

WAKATI Chama cha Wananchi (CUF) kikitupa tuhuma kwa wafuasi wa Prof. Ibrahim Lipumba kwamba, wanateka viongozi wao, wafuasi hao wamepuuza tuhuma hizo, anaandika Pendo Omary.

CUF inamtuhumu Prof. Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwamba, anashiriki mikakati ya kuhujumu harakati pamoja na kuteka viongozi wa chama hicho.

Joram Bashange, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho anadai Prof. Lipumba na kundi lake walipanga kumteka kwa lego la kumdhuru, jaribio ambalo limeshindikana.

Akizungumza na wanandishi wa habaru leo kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam Bashange amedai, Prof. Lipumba anatumia walinzi wake ambao ni Mohamed Ibrahim (mlinzi mkuu) na Shaibu Ally (mlinzi msaidzi) pia wafuasi wake Samweli Richard na Ramadhan Said kukamilisha mipango ya kumteka.

Mtandao haukufanikiwa kumpata Prof. Lipumba baada ya simu yake kuita bila kupokewa. Hata hivyo Abdul Kambaya, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho aliyefukuzwa amesema, CUF inajipa mamlaka isiyonayo.

“Jambo la kuteka ni kesi ya jinai, viongozi wa CUF waache kuchukua kazi ya polisi. Kesi inazungumzwa na RPC wa eneo husika, wanapata wapi mamlaka ya kuzungumza?

“Iwe wamemtaja Kambaya ama la, RPC ndio anapaswa kuzungumza. Mimi sijaitwa na polisi kuhojiwa,” amesema Kambaya ambaye anatajwa kuwa mtu wa karibu wa Prof. Lipumba.

Akielezea mkasa ulivyokuwa, Bashange ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF amesema “jana majira ya saa 1.30 asubuhi nikitoka nyumbani kwangu Mtaa wa Madenge, hatua 20 tu niliona gari aina ya Noah yenye namba za usajili T 760 CEF ikiwa na watu wanne ndani.

“Mtu mmoja akashuka akanionesha kitambulisho, akijitambulisha ni askari wa Kituo cha Polisi Buguruni na kunitaka niingie kwenye gari.

“Nilipomchunguza vizuri, nikamgundua kuwa ni mmoja kati ya walinzi wa Prof. Lipumba, nikagoma kuingia kwenye gari. Wakatumia nguvu kuniingiza huku wakinishambulia,” anasema Bashange na kuongeza;

“Nilipiga kelele na kuhamasisha wananchi. Wananchi wakaweka magogo na mawe, wakaizuia gari isitoke kisha wakawadhibiti hao vijana lakini mmoja alifanikiwa kukimbia. Nikatoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni na kupewa RB Na. BUG/IR/ 5937/2016.”

Mashange amesema, baada ya kutoa taarifa polisi walifanikiwa kuwakamata vijana hao ambao walikuwa chini ya ulinzi wa wananchi. Hata hivyo baada ya kukaguliwa walikutwa na pingu na vitambulisho bandia vya Jeshi la Polisi.

“Mpaka sasa Samwel Richard ambaye alikuwa dereva, Ramadhani Said na Saibu Issa wanasikiliwa na Jeshi la Polisi. Hii tafsiri yake ni nini? Prof. Lipumba alienda Rwanda kufanya utafiti wa Kiintarahamwe.

“Sasa amerudi, anafundisha watu kufanya kazi za uhalifu wa watu na kuua. Prof. Lipumba mkono wake unacheza, tuna taarifa zote,” amesema Mashange.

Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya muda ya chama hicho amesema “tunazo taarifa za kikao cha vijana kadhaa waliokuwa wameandaliwa kutudhuru. Vikao kadhaa vinafanyika nyumbani kwa Lipumba. Tunataka Jeshi la Polisi lichukue hatua. Vinginevyo tutachukua hatua wenyewe.

“Alienda Rwanda baada ya kujiuzulu. Kule kuna Intarahamwe. Ameanza kazi za kiintarahamwe katika chama chake. Tunasikitika Lipumba huyu leo ndio anaongoza magenge ya kuteka watu.

“Lazima Prof. Lipumba afahamu haya yanayoendelea tunayafahamu. Tunajua. Na vikao wanavyokaa tunajua,” amesema Mtatiro.

Mtatiro amesema haiwezeani kwamba walinzi wa wake wafanye matukio hayo halafu yeye asijue. Wanajua anajua kwa sababu vikao vinavyofanyika nyumbani kwake kila siku, hao vijana wapo na wanashiriki.

 

error: Content is protected !!