Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Wafuasi Chadema wataka fedha za faini zijenge ofisi
Habari za Siasa

Wafuasi Chadema wataka fedha za faini zijenge ofisi

Ofisi ya Chadema Makao Makuu, Dar es Salaam
Spread the love

 

WAFUASI na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameshauri kiasi cha Sh. 350 milioni kilichoshauriwa na mahakama kurejeshwa kwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho na wenzake, zitumike kujenga ofisi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Fedha hizo zilitokana na michango ya wafuasi wa Chadema kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi hao waandamizi, katika hukumu ya Kesi ya Jinai 112/2018.

Wito huo umetolewa kupitia mtandao wa Twitter, baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, kuomba maoni ya wadau, juu ya matumizi ya fedha hizo.

Mnyika alitoa wito huo kutokana na mvumo wa wafuasi hao kuhusu matumizi ya pesa hizo baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kupitia Jaji Irvin Mgeta, kubatilisha hukumu hiyo na kuamuru fedha hizo zierejeshwe kwa warufani.

Mahakama hiyo ilibatilisha hukumu hiyo iliyotolewa tarehe 10 Machi 2020 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya Mbowe na wenzake wanane, waliohukumiwa  adhabu hiyo, kukata rufaa.

Warufani wengine katika rufaa hiyo walikuwa ni Katibu Chadema, John Mnyika na Naibu Katibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Wengine ni Halima Mdee (aliyefukuzwa uanachama), Ester Bulaya (aliyefukuzwa uanachama), Esther Matiko (aliyefukuzwa uanachama), John Heche aliyekuwa mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini.

Kwa sasa Chadema imepangisha baadhi ya nyumba kwa ajili ya kufanya ofisi zake, katika Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mkoa wa Dar es salaam.

Kwenye ukurasa wa twitter wa Mnyika, Tony Alfred alishauri fedha hizo zitakapotolewa, zianze ujenzi wa ghorofa kwa ajili ya ofisi za Makao Makuu ya Chadema. Kisha wanachama watachangia fedha zilizobakia.

“Ofisi Makao Makuu, ghorofa safi, yenye nafasi ya kutosha kwa siasa za sasa na zijazo, mtuletee tuongezee itakapofikia. Au mtafute eneo jipya mjenge ukumbi mkubwa wa kutosha hata 10,000 na ofisi kwa pamoja,” ameandika Alfred.

Obed Jamel alishauri “waongeze nyumba ya pili hapo Kinondoni, ziungane kiwanja kimoja zivunjwe lijengwe jengo refu la biashara na Makao Makuu ya Chadema Taifa, tutajenga uwezo tunao.”

Naye aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph alishauri fedha hizo zitumike kununua kiwanja Dodoma, kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Chadema.

“Kwa upande wangu naomba mnunue kiwanja kikubwa Dodoma, kwa ajili ya ujenzi wa Chadema HQ ikiwa ni pamoja na ukumbi mkubwa wa mikutano. Nina amini kwa pamoja tunaweza kujenga kwa nguvu zetu bila ruzuku,” ameandika Joseph.

Wazo la Joseph liliwiana na wazo la Ryan Cykrest aliyeandika “kilichotokea leo tukiweke kwenye kumbukumbu kwa kufanya kitu kitakachoonekana na hizo fedha. Wazo langu inunuliwe eneo litakaloweza kujenga ukumbi utajaojumuisha na ofisi ya makao makuu ya chama, iwe Dodoma au Dar es Salaam.”

Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Makeba, aliandika “hizi pesa zilitolewa na wapenzi na wanachama wa Chadema na baadhi ya Watanzania wanaopenda mabadiliko, nadhani pesa zielekezwe kwenda kujenga na kuimarisha chama. Kama chama tunahitaji jengo la chama makao makuu.”

John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema

Mtu aliyejitambulisha kwa jina la Wakanda Tanzania, alishauri fedha hizo zitumike katika kukamilisha ujenzi wa ofisi za Chadema, ulianzwa kujengwa kwa fedha za wanachama.

“Pesa zote zitumike kukamilisha ofisi zilizojengwa kwa nguvu ya wanachama. Kwa maana zifanyiwe finishing (umaliziaji) na kuwekewa furniture (samani),” ameandika Wakanda

Katika hukumu hiyo, iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, ilitoa kifungo cha miezi mitano jela au faini ya Sh. 350 milioni, baada ya Mbowe na wenzake kuwekwa hatiani katika mashtaka ya uchochezi na kufanya maandamano bila kibali.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo aungana na wananchi ujenzi maabara za sekondari

Spread the loveMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na...

Habari za Siasa

CCM apiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye mambo ya kimila

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari za Siasa

Ofisi za mabalozi wa mashina zitumike kuwale vijana kimaadili – Chongolo

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza...

Habari za Siasa

Vijana ACT-Wazalendo Dar wampa tano Rais Samia

Spread the love  NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo, kimempongeza Rais...

error: Content is protected !!