January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyakazi waachwa njia panda

Maandamano wa wafanyakazi katika sikukuu ya Mei Mosi mwaka huu

Spread the love

PAMOJA na wafanyakazi kumtega Rais Jakaya Kikwete, aongoze kima cha chini cha mshahara kufikia Sh. 315,000 kwa sekta ya umma, Sh. 220,000 kwa sekta binafsi na kupunguza kodi ya mapato toka asilimia 12 hadi tisa, majibu yake hayakutoa mwelekeo kama itawezekana. Anaandika Pendo Omary …(endelea).

Katika hotuba ya Rais kwa wafanyakazi hao, iliyofanyika jijini Mwanza, Kikwete amesema “kiwango hicho kitaongezwa baada ya serikali kuangalia hesabu wakati wa kuwasilisha bajeti yake ya 2016/16.”

“Tumejitahidi kuongeza mishahara kila mwaka. Ongezeko ni dogo lakini si haba. Mwaka huu, tutaongeza tena. Kwa upande wa sekta ya umma tutaangalia hesabu kama tutafikia Sh. 315,000. Kama hatutafikia itakuwa ni kidogo,”amesema.

Kuhusu ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa sekta binasi, Rais Kikwete amesema, Bodi za Mishahara za kisekta ndizo zinahusika katika kushughurikia suala hilo.

“Bodi za mishahara za kisekta zinakutana kila baada ya miaka mitatu. Mara ya mwisho kukutana ilikuwa mwaka 2013. Mwakani zitakutana tena. Zitashughurikia suala hili,”ameeleza Rais Kikwete.

Aidha, Rais Kikwete amesema kwamba kuhusu punguzo la kodi ya mapato inayokatwa kwenye mapato ya wafanyakazi, serikali imekuwa ikipunguza mara kwa mara na itaendelea kupunguza.

“Tulikuta kodi ikiwa ni asilimia 18.5. Sasa ni asilimia 12. Mwaka huu tutaendelea kupunguza. Sijui kama tutafikia asilimia tisa. Kama tutabakisha kufikia asilimia tisa itakuwa ni sehemu ndogo sana,” amefafanua.

Rais Kikwete alikuwa akijibu hotuba ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), iliyosomwa na Katibu Mkuu wake, Nicholaus Mgaya, akiitaka serikali ya Rais Kikwete, iongeze kima cha chini cha mishahara na kupunguza kodi ya mapato.

Mgaya amesema changamoto nyingine zinazowakabili wafanyakazi ni baadhi yao kukosa uhuru wa kujiunga vyama vya wafanyakazi, Wakala wa Ajira kutotii maagizo ya serikali na upungufu wa ajira katika halmashauri;

Nyingine ni kutokuwepo kwa ushirikishwaji kati ya wafanyakazi na waajiri, ukosefu wa ajira, ajira za wageni kukosa udhibiti, kutetereka kwa amani ya nchi na ukuaji wa uchumi usiokuwa na manufaa kwa wengi.

“Ukuaji wa uchumi haujaleta manufaa kwa wafanyakazi. Kuna mgawanyo usio na udhibiti. Wapo watu wachache kwa kutumia nyadhifa zao ndio wananufaika na ukuaji wa uchumi,”amefafanua Mgaya.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Mfanyakazi jiandikishe, kura yako ina thamani kwa maendeleo yetu.”

error: Content is protected !!