January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyakazi Tanesco wapunguzwa kazini

Spread the love

ZAIDI ya wafanyakazi 39 wa Kampuni ya Jyoti Structure Ltd, mjini hapa  ambayo inasimamia mradi wa umeme chini ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wamedai kupunguzwa kazi na uongozi wa kampuni hiyo bila sababu za msingi. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Mbali na kusimamishwa kazi, wafanyakazi hao wamesema wanasikitishwa na kitendo cha kampuni hiyo kuwaondoa wao huku wakiwaajiriwa Wahindi katika kampuni hiyo.

Wafanyakazi hao walitoa malalamiko hayo mjini hapa wakati wakizungumza na waandishi wa habari na  kueleza jinsi uongozi wa kampuni hiyo unavyo wanyanyasa.

Mmoja wa wafanyakazi hao ambaye ni kiongozi wao, Issa Shaaban amesema kuwa wanasikitishwa na kitendo cha kampuni hiyo kutowathamini kwani imekuwa ikawalipa mishahara kwa kiwango cha Sh. 280,000 ambacho hakistahili kama  Serikali inavyoelekeza kima cha chini kiasi cha Sh. 325,000 ikiwemo kutowapa mikataba.

“Licha ya kufanya kazi lakini pia ulipaji wa mishahara umekuwa wakusuasua ambapo kazi tunazofanya ni ngumu na baadae uongozi huu ukaamua kutupunguza  kazi tangu Desemba 29 mwaka jana ambapo na mshahara wa mwezi huo wa Desemba hatujalipwa kabisa.

“Tumeambiwa tumepunguzwa kazini bila kupewa kiambatanisho chochote kuhusu mishahara yetu  kwa madai kuwa baadhi ya vitengo kazi zimepungua na vitengo vingine kazi zimeisha jambo ambalo sio la kweli kwani siku za hivi karibuni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na madini Dk. Medard Kalemani alipotembelea mradi huo,alieleza kuwa asilimia sabini ya mradi bado haujakamilika, Je hii ni haki?” Amehoji Shaaban.

Idrissa Khalid abaye naye ni mfanyakazi katika kampuni hiyo amesema kuwa wanashangazwa na kitendo cha kampuni hiyo kuwapunguza kazi wao ambao wanatoka mikoa mbalimbali na kuamua kuawaajiri Wahindi zaidi ya 200 kwa kazi zile zile ambazo walikuwa wakizifanya wao.

“Kampuni ya Jyoti ilitueleza kuwa kazi za kufanya zimeisha na badala yake ikatuondoa sisi wazawa na kuwaajiri Wahindi wenzao na kufanya kazi za kuokota boliti pamoja na kukoroga zege,” amesema Shaaban.

Wafanyakazi hao waliodai kupunguzwa kazi na Kampuni hiyo ya Jyoti iliwapunguza kazi mara ya kwanza na kwamba hiyo ni mara ya pili na kudai kuwa huo ni unyanyasaji kwani Wahindi ambao wanaajiriwa wanapangiwa hadi nyumba za kulala huku wao ambao ni wazawa wakiendelea kunyanyasika.

Wamesema kuwa wafanyakazi ambao ni vibarua wamekuwa wakilipwa kiasi cha Sh. 8,000 kwa siku fedha ambayo ni ndogo haikidhi mahitaji kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Aidha wafanyakazi hao walimuomba Rais John Magufuli kuingilia kati suala hilo ili kuweza kubaini vitendo viovu ambavyo vimekuwa vikifanywa na kampuni hiyo kwa wafanyakazi wazawa.

Alipotafutwa Afisa utumishi wa Kampuni hiyo, Thomas Mkwe ili kuzungumzia malamiko hayo alikanusha madai ya kuwapunguza kazi wafanyakazi katika kampuni hiyo.

“Mimi ninachofahamu mpaka sasa hivi hakuna mfanyakazi yeyote ambaye amepunguzwa kazi ila kama utahitaji maelezo zaidi uje ofisini na  muhusika upate maelezo au maswali na majibu  zaidi,” amesema Mkwe.

error: Content is protected !!