June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara wa Kongo kurejea bandari ya Dar

Bandari ya Dar es Salaam

Spread the love

SUMAIL Edward, rais wa chama cha wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kuwa wataanza kutumia tena bandari ya Dar es Salaam, kwaajili ya kusafirisha mizigo yao baada ya kusitisha kuitumia bandari hiyo kwa muda, anaandika Charles William.

Edward amewambia wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuwa, wanarudi kuitumia tena bandari hiyo baada ya serikali ya Tanzania kupunguza mizani na kodi amabazo ziliwafanya walipe fedha katika kila kituo mizigo yao inapopitia.

“Tuliikimbia bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu Tanzania baada ya wafanyabiashara wetu kuona wanabanwa sana kutokana na ushuru wa forodha, waliamua mpaka kutumia njia za panya lakini kwasasa tunaamini kodi hii itapungua na tutakaa na serikali ili kutatua tatizo hilo,” amesema.

Edward ameeleza kuwa wafanyabiashara wa Kongo wanapenda kufanya biashara na watanzania kutokana na ukarimu wao pamoja na matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa ni rahisi zaidi kueleweka kwao huku akisisitiza kuwa wanaamini mambo yataenda vyema kwa pande zote mbili.

“Tumeingia makubaliano na mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wametuhakikishia kuwa ulinzi na usalama wa  mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo inapokuwa bandarini utakuwa wa kutosha na hivyo kuanzia mwezi Novemba mwaka huu tutaanza kuleta mizigo yetu kupitia bandari ya Dar es Salaam,” amesema.

error: Content is protected !!