January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara viwanja vya Biafra watimuliwa

Spread the love

WAFANYABIASHARA wanaofanya shughuli zao katika viwanja vya Biafra vilivyopo Kinondoni wamezuiliwa kuendelea na biashara katika eneo hilo kutokana na wamiliki wa eneo hilo ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulitaka eneo kwaajili ya kuliboresha. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumzia zoezi hilo linaloendelea leo na mtandao huu, Katibu wa CCM Kata ya Kinondoni Loyce Edward amesema, utawala umeamua kuwaondoa wafanyabiashara hao kutokana na kutokaa katika mpangilio na hivyo kulichafua eneo na kulitumia kinyume cha matarajio.

Edward amesema, awali viwanja vya Biafra ambavyo CCM ndio wamiliki waliliteuwa kwa ajili ya matumizi ya umma kama kucheza mpira, mazoezi na mikutano lakini si kwa biashara zisizo katika mpangilio.

Amesema, wafanyabiashara wa viwanja vya Biafra wamekuwa wakaidi kila mara wanapotakiwa kufika katika ofisi husika ili kupata utaratibu wa kufanya biashara katika eneo hilo, lakini waliamua kujimilikisha eneo hilo kwa kupeana nafasi bila kutambua nani mmiliki halali wa eneo.

“Zoezi la kuwaondoa na kusafisha eneo hilo ulikuwa ni mpango wa muda mrefu, hivyo muda umefika na tunataka kuyaboresha mazingira ya eneo letu ili kuendana na kasi ya Rais Magufuli ya kusafisha mazingira.

“Tuna mpango wa kuweka uzio, ili eneo hilo litumike kama zamani kwa michezo na mikutano. Kama kuna wafanyabiashara ambao watapenda kufanya biashara basi watafuata utaratibu kwa kujiorodhesha na watalipa kodi,” amesema Edward.

Aidha, amewataka wafanyabiashara kwa hiari yao waondoe vifaa vyao mapema kabla hatua kali dhidi yao kuchukuliwa. “Kulikua na gereji hapa, wauza vitanda, maegesho ya magari yasiyo na mpangilio, ambavyo havitakiwi tena,” ameongeza Edward.

Hata hivyo, Mtandao huu ulizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo, huku wakiwa katika pilikapilika za kuhamisha vibanda vyao walisika wakisema, “Serikali inatakiwa kutufukilia na sisi wafanyabiashara wadogo kwa kutupa maeneo yetu.

“Hapa hatujui tunaenda wapi kufanyia biashara zetu wakati tunafamilia, tunaendesha familia zetu kwa biashara hizi. Sasa leo hii ukimwondoa mtu hapa akikosa kazi ndio anaenda kuwa kibaka mitaani kwani kapoteza ajira yake.” Wamesema wafanyabiashara hao.

error: Content is protected !!