January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara soko la Stereo walia na halmashauri

Spread the love

WAFANYABIASHARA wa Soko la Temeke Stereo, Dar es Salaam wameiomba Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kutatua changamoto zinazowakabili hasa ubovu wa miundombinu inayoathiri shughuli zao za kila siku. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Soko la Stereo ambalo hutoa huduma zake kwa wakazi wa Wilaya ya Temeke linakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ikiwa ni pamoja na mabanda chakavu ya wafanyabiashara wa kuku, mama na baba lishe, kuziba mifereji ya maji taka tatizo lililosababisha maji hayo kukosa muelekeo hivyo kutuama.

Licha ya changamoto ya uchakavu wa miundombinu, soko hilo linaelemewa na idadi kubwa ya wafanyabiashara ambao hawana sehemu maalumu za kufanyia biashara zao.

Akizungumza na MwanaHalisi Online Mwenyekiti wa Soko la Stereo, Ahmed Juma Mlemi amesema kuwa soko linakabiliwa na changamoto nyingi kwa kipindi kirefu kabla kuingia madarakani lakini hadi sasa changamoto hizo hajitafutiwa ufumbuzi.

“Hali ya soko letu hairidhishi, tunakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu, tatizo hili lilianza kulalamikiwa kabla ya uongozi uliopo, cha kusikitisha halmashauri haijachukua hatua za kutatua changamoto hizi,” amesema Mlemi na kuongeza;

“Soko hili sasa limepanuka, lina wafanyabiashara wengi ambao hawana maeneo maalum ya kufanyia biashara zao, tuliiomba halmashauri kuwasaidia kujenga vibanda kwenye sehemu zilizowazi ili wapate maeneo salama lakini hadi sasa hatujasaidiwa,” amesema Mlemi.

Mlemi alidai tatizo linalochangia changamoto zao kutotatuliwa haraka ni ukosekanaji wa ushirikiano baina ya wafanyabiashara na halmashauri na kwamba imekuwa ikiwakwepa.

“Kutopewa kipaumbele kwa viongozi wa soko ndiyo mzizi mkuu wa tatizo, Halmashauri haitoi ushirikiano wa dhati kwetu. Kila wakija huwafuata viongozi waliowaweka ambao hawazijui changamoto zetu,” amesema.

“Wafanyabiashara tunamchango mkubwa kwenye halmashauri yetu na tunazijua njia za kutatua changamoto zetu ila hatupewi kipaumbele, tunajitahidi kuliboresha soko ila halmashauri haiongezi nguvu,” amesema na akuongeza;

“Wafanyakazi wa soko wanafanya usafi kila siku ila taka zinazokusanywa kwenye kizimba cha taka hazitolewi kwa wakati, inatakiwa kila siku kijiko na gari za taka zije kuzoa lakini linakuja gari moja wakati mwingine kijiko hakiji kuzoa taka wanabaki wafanyakazi wachache ambao hawana vifaa vya usalama wa afya zao wanapozoa taka,wazoaji pekee hawawezi kuzimaliza taka zote,”amesema Mlemi.

error: Content is protected !!