October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara soko la kuku Dodoma wapewa angalizo

Spread the love

WAFANYABIASHARA wa soko la kuuza na kuchinja kuku lililopo Mwembe Tayari, jijini Dodoma wametakiwa kufanya biashara hiyo kwa kuzingatia kanuni na sheria za usafi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na James Yuna, Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma alipofanya ziara katika soko hilo. Amesema, katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha, ni muhimu kuzingatia zaidi usafi.

Ameeleza kuwa, kama wafanyabiashara hao hawatazingatia usafi unaotakiwa, viongozi wa jiji hawatasita kufungia biashara zao.

“Kwa sasa Dodoma ni jiji, na ni makao makuu ya nchi, wageni wanaingia kila saa, kwa maana hiyo ni lazima kuhakikisha usafi wa mazingira hususani katika masoko, unazingatiwa.

“Dodoma kuna sifa kubwa ya kuwepo kwa kuku wa kienyeji, na wageni wengi wanataka kula kuku wa kienyeji, kwa maana hiyo biashara ya kuku pamoja na machinjio yanatakiwa kuwa katika hali nzuri,” amesema na kuongeza;

“Mteja anapokuja katika soko la kuku na kumleta kuku wake hapa machinjioni, akute ni pasafi ili aondoke akiwa na furaha na hamu ya kula kuku ambaye anaandaliwa katika mazingira mazuri.”.

Pia Yuna ametoa agizo kwa viongozi wa soko hilo kutafuta muda wa kufanya vikao na wafanyabiasjara, kwa mantiki ya kuhakikisha usafi wa uhakika unafanyika ndani ya soko.

error: Content is protected !!