September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara lawamani kutoshusha bei ya Sukari

Spread the love

WAKAZI wa maeneo mbalimbali katika mji wa Dodoma wameendelea kuwalalamikia wafanyabiashara wa sukari kwa kuiuza bei ya juu licha ya serikali kutangaza bei elekezi ya sh.1800 kwa kilo, Anandika Danny Tibason

MwanaHALISI Online  iliweza kufanya mahojiano na wakazi wa Ilazo, Kikuyu, Chang’ombe,Ipagala na Ntyuka ambao kwa nyakati tofauti walisema bado sukari inauzwa kwa bei ya juu zaidi.

Mkazi wa Ilazo ambaye alijitambulisha kwa jina la Said Masudi amesema mpaka sasa sukari inauzwa kati ya sh. 2500 hadi 3500 kwa kilo.

Amesema kutokana na kuendelea kuwepo kwa bei hiyo inaonesha matumizi ya sukari kuwa anasa.

Naye mkazi wa Kikuyu aliyejitambulisha kwa jina la Yohana Mashinje ameeleza kuwa bei ya sukari kwa sasa haifanani kwani kuna wanaouza kati ya sh. 3500 hadi 4000 huku wenguine wakiuza 3000 kwa kilo.

Wakazi wa Chang’ombe,Ipagala na Ntyuka kwa nyakati tofauti walisema sukari mpaka sasa haijapatikana licha ya serikali kutangaza kuwa imeagiza sukari nyingi kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kukamata sukari nyingi ambayo imekamatwa kutoka kwa wafanya biashara ambao wanadaiwa kuwa walikuwa wameficha sukari hiyo.

Hata hivyo kwa upande wao wafanya biashara wa kuuza sukari wamesema  wanaendelea kuuza sukari kwa bei kubwa kutokana na na wao kununua bei ambayo siyo rafiki.

Wamesema wao kwa sasa wananunua sukari kwa bei ya jumla kwa sh.2500 pamoja na usafirishaji na ubebaji wanajikuta sukari ikifikia kiasi cha sh. 2800 jambo ambalo wakiuza kwa bei elekerzi kamwe hawawezi kupata faida.

Mmoja wa wafanyabiashara wa sukari kwa reja reja, Joel Chibago, amesema wanalazimika kuuza sukari hiyo kwa bei ya juu kutokana na wao kununua kwa bei ambayo siyo elekezi.

Mfanyabiashara mwingine ambaye akutaka kujitambulisha alisema kwa sasa sukari bado inauzwa kwa bei ya juu kutokana na kupatikana kwa shida.

Kwa upande wake wakala wa kusambaza sukari katika mkoa wa Dodoma, alisema yeye bado anayo skura katika ghala lake ambapo sukari hiyo inaweza kuisha kati ya jumatatu ya wiki ijayo.

Meneja wa kampuni ya H.M.H.Gulamari,Mustafa Sighi akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa Kampuni hiyo Haidary Gulamali amesema kutokana na serikali kudai kwamba wameagiza sukari kutoka nje kwa sasa wateja wake wamepungua kwani wananunua kwa machale wakijua kuwa sukari itashuka hapo baadaye.

“Kwa sasa sisi bado tuna kiasi kikubwa cha sukari ambacho tunatazamia kuwa inaweza kuisha kati ya Jumatatu ijayo,lakini bado tunaendelea na juhudi za kushughulikia ili tuweze kupata sukari ambayo serikali imeagiza nje ili kuwapatie wateja huduma hiyo.

“Pamoja na kuwa tuna sukari lakini bado wateja kwa sasa wananunua sukari kwa kusua sua kwa kutegeshea kuwa uenda sukari ikashuka zaidi kutokana na sukari iliyoagizwa kutoka nje ya nchi” amesema Sighi.

Katika mkoa wa Dodoma kada wa CCM ambaye ni wakala wa usambazaji wa sukari katika mkoa huu alilazimishwa kusambaza sukari hiyo kwa madai kuwa alikuwa ameifungia kwa lengo la kuificha.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana akiwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alitoa tamko la kuwataka wale wote walioficha sukari majumbani kuifichua mara moja na wasipofanya hivyi watachuliwa hatua.

Pamoja na kauli hiyo ya Rugimbana bado haijaweza kutolewa maelezo kama wamekamata sukari nyingine iliyofichwa au la.

error: Content is protected !!