August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wafanyabiashara ‘kufunga’ biashara zao

Maduka ya jijini Mwanza yakiwa yamefungwa kutokana na mgomo uliowahi kutokea siku za nyuma

Spread the love

WAFANYABIASHARA wa maduka ya nguo za jumla na rejareja katika Jiji la Mwanza, wametishia kufunga biashara zao kutokana na Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, kupandisha tozo pamoja na ushuru wa biashara zao bila kuwashirikisha, anaandika Moses Mseti.

Hali hiyo, imesababisha baadhi ya wafanyabiashara hao wanaofanyia shughuli zao katika mtaa wa Liberty, kuingia katika mgogoro na mkurugenzi Kibamba, kutokana na ongezeko la tozo huku wengine wakilalamikia utaratibu wa ulipaji wa tozo kwamba unafanyika kinyemera.

Baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema wengi wao hawajapewa elimu juu ya ongezeko hilo la kodi ya ushuru lakini walishangaa kuona wanapelekewa notisi ya siku saba iliyowataka kulipa tozo pamoja na ushuru ndani ya kipindi hicho.

Wamesema kuwa, awali walizoea kulipia masuala yote yanayohusu kodi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku wakidai kwamba kuongezewa kodi kutasababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka kutokana na mzunguko mdogo wa biashara katika kipindi cha hivi karibuni.

“Mgogoro huu umesababisha wenzetu wanne wakamatwe na Polisi tangu Juni 30 mwaka huu baada ya kushindwa kulipa ushuru na sasa wanaendelea kusota katika mahabusu ya gereza la Butimba kwa kushindwa kulipa tozo za halmashauri ya Jiji,” amesema Elizabeth Mnubi.

Mnubi amewataja wafanyabiashara wanne wanaoendelea kusota katika gereza hilo, kuwa ni Ganta Ngamaya, Nicolaus Hezwa, Mariam Saizi na Joyce Benedicto ambao mpaka sasa hawajui hatima yao kutokana na kunyimwa dhamana Polisi.

Mnubi ameongeza kwamba, barua ya notisi ya siku saba iliyopelekwa kwa wafanyabiashara hao iliandikwa kwa lugha ya kingereza huku wafanyabiashara walio wengi hawafahamu lugha hiyo na pia hawana wanasheria wanaoweza kuwasaidia kuitafsiri barua hiyo.

Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji hilo, alipotafutwa leo saa 10 : 30 asubuhi ofisini kwake ili kuzungumzia suala hilo hakuwepo hata alipopigiwa simu yake ya kiganjani haikupatika

Machi 22 mwaka huu, mkurugenzi huyo, kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba. F. 20/70/ IV alitoa notisi ya siku saba kwa wafanyabiashara wote ambao hawajalipa tozo na kodi za serikali kufanya hivyo mara moja bila kuchelewa vinginevyo waliarifuwa kwamba wangefungiwa maduka yao bila maelezo ya ziada ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wafanyabiashara hao wamefikishwa kwenye vyombo vya dola kinyume cha kifungu cha 35 na 36 vya sheria ya fedha na namba 8 ya mwaka 2012 inayosomwa pamoja na sheria ndogo namba 4 ya mwaka 2012 ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza dhidi ya watu wanaokwepa kulipa ushuru wa serikali kwa halamshauri ya jiji hilo.

error: Content is protected !!