WADHAMINI wa Tundu Lissu, leo tarehe 20 Februari 2020, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jiijini Dar es Salaam kutoa hati ya kumkamata mdaminiwa wao (Lissu). Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Ibrahim Ahmed na Robart Katula, wameieleza mahakama kwamba, juhudi zao za kumfikisha mahakamani hapo Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki zimegonga mwamba, na sasa wanaiomba mahakama kuwasaidia.
Maombi ya wadhamini hao, yamefikishwa wakati shauri hilo lilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Awali, wakili wa serikali mwandamizi Wankyo Simon, amedai upande wa mashtaka umepokea maombi kutoka kwa wadhamini wa mshtakiwa huyo, ya kuomba kumkamata ili waweze kujitoa kwenye udhamini huo.
Wankyo amedai, upande wa mashtaka umeridhia kusikilizwa maombi hayo, ambapo wameomba yasikilizwe kesho tarehe 21 Februari 2020.
Katula amedai kuwa, wameshindwa kumkamata na kumleta mshtakiwa huyo kwa nguvu zao, hivyo wanaomba kusikilizwa kwa maombi hayo.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba amehairisha shauri hilo kesho, ambapo pande zote zitakuja kuangalia taratibu za kisheria juu ya maombi hayo na kusisitiza kuwa, amri za kesi ya msingi bado zinaendelea kuwa na nguvu.
Mbali na Lissu, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Simon Mkina, ni mhariri wa gazeti la MAWIO; Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mehbob, mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji ya magazeti ya Jamana. Wanakabiliwa na mashitaka matano katika mahakama hapo, likiwamo uchochezi.
Wote wanne, wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002. Habari ambayo inadaiwa kuwa ya uchochezi, ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Machafuko yaja Zanzibar.
Leave a comment