September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wadhamini wamgeuka Tundu Lissu

Spread the love

YAMEWAFIKA shingoni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wadhamini wa Tundu Lisuu, Robert Katula na Ibrahim Ahmed ‘kuja juu,’ kutokana na kauli ya mdhaminiwa wao, kwamba anawahurumia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

“Tundu Lissu hatuonei huruma, sababu haoneshi ushirikiano. Tangu tarehe 6 nimemtumia sms (ujumbe mfupi wa maneno) kuhusu kuzungumza suala hili, lakini hajatoa ushirikiano,” amesema Katula.

Katula na Ibrahim wametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Januari 2020, ikiwa ni siku moja baada ya Thomas Simba, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam kusema ‘anaweza kuwachukulia hatua wadhamini hao.’

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tayari amesema, kwamba hana namna nyingine ya kuwasaidia wadhamini wake huku wadhamini hao wakikabiliwa na kiwewe cha pingu katika mahakama hiyo.

“Kama angekuwa anatuhurumia, angetupa ushirikiano ikiwemo kurejea nchini, ili aendelee na kesi yake,” amesema Katula na kuongeza:

“Sisi tulimdhamini kwa muda, ilitakiwa alete wadhamini wa kudumu lakini ilishindikana. tulimdhamini kwa sababu kesi ilikuwa inahusiana na gazeti letu la Mawio.”

Lissu anatuhumiwa kwenye kesi hiyo ya uchochezi sambamba na watuhumiwa wengine watatu, ambao ni Simon Mkina, mhariri wa gazeti la MAWIO; Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mehbob, mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji ya magazeti ya Jamana.

Wote wanakabiliwa na mashitaka matano katika kesi namba Na. 208/2016, likiwamo uchochezi. Wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Habari ambayo inadaiwa kuwa ya uchochezi, ilibeba kichwa cha maneno kilichosema ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katula amesema, walikuwa wadhamini wa muda, kwa kuwa walikubaliana, kwamba Lissu atafute wadhamini wa kudumu, lakini mchakato huo ulikwama baada ya mtuhumiwa huyo kujeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana tarehe 7 Septemba 2017, Dodoma na kupelekwa nje kwa matibabu.

“Sisi tulikuwa wadhamini wa muda, na makubaliano yetu ilitakiwa alete wadhamini wa kudumu, ambao ni ndugu zake wanaojua hata akitoroka, wanampatia wapi.

“Lakini mchakato huo ulikwama baada ya yeye kupigwa risasi na kuondoka nje ya nchi, ndio changamoto hii ilivyotokea,” ameeleza Katula.

Ahmed amesema, kitendo cha Lissu kutowapa ushirikiano kinawaweka katika mazingira magumu, kutokana kwamba Hakimu Simba amewapa amri ya kumleta mahakamani hapo tarehe 20 Februari 2020, na kama hawatafanya hivyo, atawchukuliwa hatua.

“Mahakama itachukua uamuzi kama tukishindwa kumpeleka mahakamani. Na wadhamini tunapowasiliana na Lissu ili afike mahakamani, haoneshi ushirikiano wa kurudi nchini,” amesema Ahmed.

Kufuatia changamoto hiyo, wadhamini hao wamesema, waliamua kumwandikia barua Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, ili kumshawishi Lissu kurejea nchini kwa ajili ya kufika mahakamani.

“Tumeandika barua tangu tarehe 10 Januari mwaka huu, na namba zetu za simu tumeweka tukiamini, kwamba watatutafuta ili kushughulikia suala hili, lakini isivyo bahati hadi leo kimya, Mbowe hajatujibu, licha ya kwamba barua ile ilifika ofisini kwake,” amesema Ahmed.

Akizungumza na mtandao huu jana tarehe 20 Januari 2020, Lissu ambaye ni Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), amesema msalaba kuhusu kesi hiyo ni wa kwake mwenyewe na si wa Mbowe wala Chadema.

“… msalaba wangu wa kijinai, kama upo, hauwezi kubebwa na Mh. Mbowe au Chadema au na mtu mwingine yeyote,” amesema.

error: Content is protected !!