April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wadhamini wa Lissu wabanwa mahakamani 

Tundu Lissu, Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewataka wadhamini wa aliyekuwa mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, kupeleka udhibitisho mahakamani kuhusu afya yake. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, aliagiza wadhamini hao, Robert Katula ambaye ni Meneja Mkuu wa kampuni ya Hali Halisi Publshers Limited (HHPL) na Ibrahim Ahmed, ofisa usambazaji wa kampuni hiyo, kufika mahakamani hapo, tarehe 21 Novemba 2019, wakiwa na ushahidi huo.

Simba alitoa kauli hiyo, baada ya Katula kuieleza mahakama kuwa Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, bado anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji.

Lissu na wenzake watatu – Simon Mkina, mhariri wa gazeti la MAWIO,  Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo naIsmail Mehbob, mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji ya magazeti ya Jamana – wanakabiliwa  na mashitaka matano mahakamani, likiwamo uchochezi.

Wote wanne, wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, watuhumiwa walitenda kosa hilo jijini Dar es Salaam. Habari ambayo inadaiwa kuwa ya uchochezi, ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Machafuko yaja Zanzibar.”

Katika shitaka la pili, washatakiwa wote wanne, wanadaiwa kuwa  14 Januari 2016, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Shtaka la  tatu linamkabili mshtakiwa wa tatu, Mehboob  ambaye anadaiwa kuwa 13 Januari 2016, katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala,  jijini Dar es Salaam, alichapisha gazeti la MAWIO lililokua na taarifa za uchochezi.

Mshitakiwa huyo alidaiwa pia  alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Shitaka la tano linawakabili washtakiwa wote kwa pamoja ambao wanadaiwa kuwa  tarehe 14 Januari 2016,  bila ya kuwa na mamlaka yoyote,  waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu.

Awali Estazia Wilson, wakili mwandamizi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa kuwa upelelezi wake tayari umekamilika.

Hata hivyo, Wilson alisema, kesi hiyo haitaweza kuendelea mpaka pale afya ya Lissu itakapoimarika; ndipo Hakimu Simba aliposema, “mdhamini wa Lissu atuletee udhibitisho wa afya yake ili tuweke kwenye rekodi.”

Baadhi ya wanasheria wameiambia MwanaHALISI ONLILE kuwa uendeshaji wa kesi hiyo mahakamani, utaibua mambo kadhaa, likiwamo suala zima la mahakama kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa sababu wahusika ni  Zanzibar na siyo Tanzania Bara.

“Sheria ya Magazeti haiko kwenye Sheria ya Muungano. Mambo haya yanatarajiwa kuibuka mahakamani na kuweza kuibua mivutano ya kisheria. Lakini yote kwa yote, tusubiri muda wa kusikiliza kesi utakapofika,” ameeleza.

Lissu alishambiliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2019, akiwa nyumbani kwake eneo la ‘Area D’ jijini Dodoma na kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Nairobi nchini Kenya ambapo tarehe 6 Januari 2018 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo yupo mpaka sasa.

Shambulizi dhidi ya Lissu, lilitokea muda mfupi baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge wa asubuhi.

error: Content is protected !!