Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wadau wataka mjadala wa kitaifa matokeo ya sensa
Habari za SiasaTangulizi

Wadau wataka mjadala wa kitaifa matokeo ya sensa

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Anna Makinda
Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeshauriwa kuitisha mjadala wa kitaifa kuhusu takwimu za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, ili kubaini mahitaji halisi ya wananchi, kwa ajili ya kuyatimiza. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo umetolewa leo Jumatano, tarehe 2 Novemba 2022 na wadau mbalimbali wakizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, kuhusu matokeo ya awali ya sensa iliyofanyika Agosti 23 mwaka huu.

Ushauri huo umekuja baada ya matokeo hayo kuonyesha idadi ya watu imeongezeka mara tano, kutoka milioni 12.3 iliyokuwa 1967, hadi kufikia milioni 61.7, kwa mwaka 2022.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)- Dayosisi ya Karagwe, Askofu Benson Bagonza, amesema inabidi wataalamu waketi kwa ajili ya kujadili huduma zinazotolewa kwa wananchi ili kuweka viwango vya huduma halisi zinazohitajika, hususan za elimu na afya.

“Kwanza niseme kwamba takwimu hizi zinahitaji mjadala wa kitaifa, inabidi wataalamu tukae tujadili na kuweka viwango ndipo tuweze sema zinahitajika hospitali ngapi. Sababu ulimwengu wa Sasa si vizuri kuwa na vituo vya afya kwa ajili ya kutibu wagonjwa, tunahitaji vituo vinavyozuia ugonjwa kuliko kuponya. Ili hayo yaweze kufanyika tunahitaji mjadala,” amesema Askofu Bagonza.

Kiongozi huyo wa kiroho amesema “huwezi kukurupuka katika utekelezaji wa jambo lolote bila mjadala wenye mikakati sababu dunia ya sasa hatuhitaji kuzungumzia habari ya magonjwa, tunahitaji kuzungumzia huduma ya chanjo za kuzuia magonjwa. Tunahitaji kupunguza idadi ya watu kukaa hospitalini.”

Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya sensa, Tanzania kuna hospitali 714, wakati vituo vya afya vikiwa 1,550, huku zahanati zikiwa 8,098.

Askofu Bagonza ameshauri Serikali iongeze idadi ya majengo ya kutolea huduma za afya, sambamba na kuziboresha, “unaweza ukawa na hospitali moja wilayani inafanya vizuri na watu wanahudumiwa kuliko kuwa na hospitali 20 halafu hazifanyi chochote.”

Kuhusu sekta ya elimu, Askofu Bagonza amesema “elimu sio majengo, tuhakikishe mjadala kuhusu mfumo wa elimu unafanyika. Tukishahitimisha mjadala kuhusu mfumo wa elimu idadi ya majengo itajulikana kama inatosha au haitoshi sababu huenda ikawa inatosha kama tungekuwa na mfumo mzuri wa elimu.”

Matokeo ya sensa yanaonesha kuwa, Tanzania Kuna shule za msingi 19,769 na za sekondari 5,857.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, ameshauri matokeo ya sensa hiyo yatumike vizuri katika kutambua changamoto zinazowakabili wananchi ili zifanyiwe kazi.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza

“Kwa sasa haya ndiyo mambo ya kufanyiwa kazi, kuja na mikakati inayotekelezeka sio kuwaambia vijana wajiajiri, watajiajiri kwa kitu gani na kwa soko lipi. Hayo ndiyo mambo ya kuangalia, baada ya sensa tukae kuona nguvu kazi tuliyonayo kama taifa tuwaandae kuwa wazalishaji,” amesema Padri Kitima.

Amesema, matokeo ya sensa yanaonesha kuwa asilimia 65 ya Watanzania wako vijijini, hivyo Serikali ijenge vituo vya afya vya kutosha vyenye wataalamu wengi na vifaa tiba, ili wapate huduma bora kuhakikisha matakwa ya Katiba ya Tanzania Ibara ya 14 inayoweka haki ya msingi kwa kila Mtanzania kuwa hai, inatimizwa kwani magonjwa yanahatarisha haki ya kuishi.

Kuhusu sekta ya elimu, Padri Kitima amesema idadi ya shule inaridhisha kidogo na kwamba Serikali inapaswa kuweka mikakati ya kutoa elimu inayomuandaa kijana kujiajiri na kuwa mzalishaji mali.

“Shughuli ya kilimo inaonesha ni eneo ambalo lingeweza pokea karibu vijana wote, wapo watakaolima, sindika mazao, kuuza mazao na haya yote bado hayajapangwa vizuri,” amesema Padri Kitima.

Wakati huo huo, Padri Kitima ameshauri sera na sheria ya sekta binafsi zitungwe, ili kuzalisha wawekezaji wa ndani wa kutosha na kuondoa utegemezi wa wawekezaji wa nje ambao wanatoa fedha nchini na kuzipeleka nje kitendo kinachoathiri uchumi wa nchi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tazania (TEC), Padri Charles Kitima

“Hatujashiriki biashara ya kimataifa ipasavyo, tunashiriki kwa kutumia rasilimali zetu za ndani na sio kutoa huduma. Kampuni za ujenzi wa barabara zinatoka nje badala ya ndani wakati tuna uwezo wa kuanzisha za kwetu na kuzibakisha fedha ndani. Hatujawaandaa wazawa kushiriki sekta binafsi matokeo yake hela inakwenda nje bila kurudi,” amesema Padri Kitima.

Aidha, Padri Kitima ameishauri Serikali kuwaandaa vijana kuwa na vigezo vya kuajiriwa nje ya nchi hususani katika sekta ya afya na viwanda, kwani ndiko kuna soko kubwa la ajira.

Kwa upande wake Msemaji wa Sekta ya Afya ya Chama cha ACT- Wazalendo, Ruqayya Mahmoud, ameishauri Serikali iongeze vituo vya afya pamoja na kuboresha huduma zake, ili kukidhi matakwa ya muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, uliowasilishwa bungeni hivi karibuni.

“Matokeo ya sensa ni mazuri, idadi ya wananchi ni kubwa kuliko vituo vya afya sababu muswada wa afya utakaoenda kupitishwa bungeni uko katika mfumo wa rufaa kwamba huwezi fika juu lazima uanzie chini. Hivyo lazima Serikali iwekeze zaidi kuongeza vituo kuliko hospitali,” amesema Ruqayya na kuongeza:

“Pia, wahakikishe huduma zinazotolewa ni nzuri sababu hivyo vituo havimudu matatizo ya wananchi. Kama Kijiji kina vituo viwili vyenye vifaa wananchi watatibiwa huko.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!