January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wadau wajadili elimu jumuishi, kuwainua wenye ulemavu

Spread the love

 

SHIRIKA la Light for the Word, limeitaka jamii ya Kitanzania kushirikiana kwa pamoja kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi ikiwemo za macho na elimu jumuishi kwa wenye ulemavu ili waendelee na masomo. Anaripoti Mwansishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza katika mkutano wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wakiwemo wa serikali, asasi za kiraia, mkurugenzi mkazi wa shirika hilo, Joseph Banzi amesema, shirika hilo linafanya kazi nan chi tatu za Afrika ambazo ni Congo, Rwanda na Tanzania.

“Tunapaswa kuhakikisha tunakuza uelewa juu ya elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu, ili tuweze kukaa pamoja na kuweka mikakati ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu kuendelea na masomo na kikubwa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu elimu jumuishi,” amesema Banzi

Amesema, wamekuwapo nchini tangu mwaka 2017 ambapo wamekuwa wanaangazia changamoto na jinsi ya kuwasaidia ili waweze kuendelea na masomo na wafikie ndoto zao na wamekuwa wakifanya kazi kwenye maeneo matatu.

“Tunasaidia katika kutokomeza changamoto ya macho hususan wasioona waweze kuona; eneo la elimu jumuishi kwa kufanya kazi na serikali na wadau mbalimbali ili watoto wenye ulemavu wanapata fursa ya kuweza kuendelea na elimu; kuhakikisha wale watu wenye changamoto ya ulemavu na changamoto zingine tunawasaidia waweze kukua kiuchumi,” amesema Banzi

Mkurugenzi huyo amesema, “watoto wengi wenye changamoto kama hizi na ama wazazi hawajui wapi wanaweza kusaidiwa, wanaweza wasiendelee na masomo. Sisi tunawatafuta huko kwenye jamii na tukiwapata tunawasaidia kwa kuwapa vifaa vya kumwezesha kuona.”

Amesema, wanafanya kazi na Hospitali bingwa kama KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro na CCBRT ya jijini Dar es Salaam, “ili kuwawezesha kupewa huduma hizi za macho.”

“Hawa watoto tunaowasaidia, wamekuwa wakifanya vizuri zaidi kwenye masomo yao. Asilimia 70 wanaofanya mitihani ya darasa la saba wanafaulu na kuendelea na masomo ya sekondari. Hivyo, tuendelee kushirikiana kwa wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye changamoto,” amesema.

Banzi amesema, elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa jamii ili kutambua na kuthamini elimu jumuishi, “kwani watu wenye changamoto ya ulemavu, asilimia kubwa wanaachwa nyuma na hata serikali inazungumzia jinsi ya kuwasaidia kiuchumi watu wenye changamoto ya ulemavu.”

“Sisi tunawafundisha na kuwaelekeza jinsi ya kutafuta fursa za kazi na tunafanya kazi kwa karibu na taasisi mbalimbali kwa njia za Intern,”amesema

Kwa upande wake, Mwenyekiti Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Ernest Kimaya, alisema “bado changamoto zipo za kupata elimu, tukikaa pamoja na kushauri jinsi ya kutatua changamoto hizi zinazosababisha watoto wenye ulemavu kutopata elimu vizuri.”

Kimaya amebainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu ni “ukosefu wa walimu wenye taaluma hiyo ya kufundisha wenye ulemavu pamoja vifaa vya kufundishia. Tukikaa pamoja tutaona jinsi ya kufanya.”

error: Content is protected !!