June 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wadaiwa Bodi ya Mikopo kutajwa majina hadharani

Spread the love

SERIKALI imepanga kutangaza kwa umma majina ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajaanza kurejesha fedha kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kufunga maonesho ya vyuo, Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi amesema kuwa majina hayo yataanza kutangazwa wiki ijayo.   

“Natoa rai kwa wote walionufaika na mikopo ya elimu ya juu, waende wakalipe mikopo yao, kwa kuwa kuanzia wiki ya kesho majina ya wadaiwa wote ambao hawajaanza kurejesha malipo yao yataandikwa hadharani,” amesema.

Amesema, wanaokwepa kurejesha mikopo yao wanasababisha baadhi ya wanafunzi wasio na uwezo kuikosa fursa ya kupata mikopo kwa wakati.

“Watambue kuwa fedha zile siyo za bodi au wizara, ni za fedha za umma na kwamba wanaposhindwa kulipa wanakwamisha wengine kupata mikopo,” amesema.

Aidha, Tarishi amesema serikali imejidhatiti kuboresha elimu ikianzia kwa kufanya mchujo wa wanafunzi wenye vigezo na sifa stahiki za kujiunga na masomo katika ngazi mbalimbali pamoja na kuboresha miundombinu.

“Serikali imepanga kuboresha miundombinu, kuongeza vifaa vya ufundishaji, maabara hususan kwa vyuo vya sayansi. Pia itahakikisha vyuo vinakuwa na waalimu mahiri ili kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora na si bora elimu,” amesema.

Amesema kuwa mikakati ya serikali ni kutoa elimu bora na ya kiwango kwa kuandaa mitaala bora, kuboresha mbinu za ufundishaji,  pamoja na kutengeneza mazingira yatakayofanya wanafunzi kuwa na utayari wa kusoma,” amesema.

Eleuther Mwageni, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) amesisitiza kuwa sifa za wananfunzi wanaomaliza kidato cha sita ambao wanastahili kujiunga na vyuo vikuu zimebadilika na kusema kuwa hivi sasa wanaochaguliwa ni wale waliofaulu kwa alama 4.

“Awali ilikuywa wanachaguliwa wanafunzi wenye alama 2 ambacho ni kwango cha ufaului wa E, lakini kwa sasa kiwango cha chini cha ufaulu ni alama 4,” amesema.

Mwageni amewaasa wanafunzi wasio na vigezo vya kujiunga na elimu ya juu wanaofikiria kwenda kujiunga na vyuo vilivyomo nje ya nchi ambavyo vinakubali matokeo yao, kwamba waache kwa kuwa nchi zote sasa zinazingatia viwango vya ufaulu vya nchi.

“Hata ukienda kusoma nje ya nchi wakati huna sifa, lazima utarudi nchini, na kwamba uangalizi hivi sasa upo wa hali ya juu kabla ya kuajiriwa vyeti vyako vitachunguzwa na uikibainika hukukidhi vigezo ni vigumu kupata ajira,” amesema na kuongeza.

“Labda uende ukafanye kazi nchi nyingine lakini ninavyojua nchi zote za Afrika Mashariki na SADC zinakubali vigezo tulivyopanga.”

 

error: Content is protected !!