KIKUNDI cha wachimbaji wadogo kinachomiliki mgodi wa dhahabu wa Kapumpa uliopo tarafa ya Kitunda wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora kimeongoza kwa kulipa mrabaha (royalty) wa zaidi ya Sh. 30 milioni serikalini kwa kipindi cha miezi mitatu kati ya migodi 617 yenye leseni, anaandika Mwandishi Wetu.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda hiyo, Salim Salim, kwa niaba ya Kamishna wa madini nchini, Benjamin Mchwampaka, katika taarifa yake juu ya uchimbaji mdogo wa madini katika kanda hiyo, alisema leseni ya kikundi cha wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Kapumpa imeongoza kwa kulipa Sh. 30.42 milioni kwa kipindi cha kati ya Mei na Julai, mwaka huu.
Aidha, leseni ya umoja wa wachimbaji wadogo wa dhahabu ya wilayani Nzega Mkoa wa Tabora imefuatia kwa kulipa mrabaha wa Sh. 24.5 milioni, huku kikundi cha madini cha Tumaini kikishika nafasi ya tatu kwa kulipa Sh 22.4 milioni .
“Leseni ya mgodi wa Shukrani Chacha Chacha wa Wilayani Sikonge umeshika nafasi ya nne kwa kulipa mrabaha wa Sh. 14.9 milioni na mgodi wa Gregory Kibusi Gallid uliopo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wenyewe umelipa Sh. 3.99 milioni,” alisema.
Leave a comment