August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Wachimbaji kamilisheni ahadi zenu’

Wachimbaji wadogo wadogo mkoani Morogoro

Spread the love

THERESIA Theodori, Kaimu Ofisa wa Madini Mkazi katika Mkoa wa Morogoro amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini wenye vibali na leseni kuwa na uhusiano mzuri na jamii inayowazunguka ili kuepusha migongano, anaandika Christina Haule.

Theodori ambaye pia ni Mjiolojia wa Madini amesema wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amewataka wachimbaji hao kujenga uhusiano mzuri na jamii kwa kuchangia huduma za maendeleo na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali.

Amesema kuwa, ili wachimbaji hao waweze kufanya kazi zao kwa urahisi na kuepuka migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kati yao na jamii, ni lazima wafuate sheria za madini zinavyowataka na kujenga utaratibu wa kutoa huduma na misaada mbalimbali sambamba na kulipa tozo za madini kwa serikali.

“Ni muhimu sana kwa Wachimbaji wadogo kutimiza ahadi zao wanazowaahidi wananchi wakati wanaanza uchimbaji na kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri ili kuepuka migogoro, hata kujitolea gari kusaidia wagonjwa au kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo” amesema.

Amesema kuwa, migogoro mbalimbai huwa inaibuka kwa wachimbaji na jamii baada ya wachimbaji kushindwa kutekeleza ahadi zao.

Aidha, amewataka wananchi kuwa wavumilivu pindi wachimbaji hao wanaposhindwa au kuchelewa kutimiza ahadi walizozitoa za kuchangia miradi ya maendeleo kwa kuwa, kuna wakati hawapati madini kama walivyotegemea.

error: Content is protected !!