February 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge zaidi kuzidi kupukutika

Rais John Magufuli akiongoza Kamati Kuu ya CCM

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewatishia wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani, kuwa kama wanataka kujiunga na chama hicho, wafanye haraka, vinginevyo wanaweza kutupwa nje. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyotolewa jijini Dar es Salaam, leo Jumanne, imeeleza kuwa wale watakaoshindwa kujiunga na CCM, katika kipindi cha wiki mbili zijazo, wanaweza wasiteuliwe kugombea tena nafasi zao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kwamba “Kamati Kuu (CC), imeelekeza kuwa 15 Novemba 2018, ndio utakuwa mwisho wa kupokea maombi ya uanachama wa CCM na kupewa dhamana ya uwakilishi kupitia tiketi ya CCM kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine.”

Inaongeza, “…baada ya tarehe hiyo, wabunge na madiwani watakaomba kujiunga na CCM watapokelewa na kubaki kuwa wanachama wa kawaida na hawataruhusiwa kugombea au udiwani mpaka itakapoamuliwa vinginevyo.”

Aidha, katika kikao hicho cha dharura, waliokuwa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika majimbo ya Simanjiro, Ukerewe, Babati Mjini na Serengeti, wameteuliwa kugombea tena nafasi hizo.

Waliokuwa wabunge wa Chadema na ambao walijiuzulu nafasi zao na kuamua kujiunga na CCM, ni pamoja na James Millya (Simanjiro); Pauline Gekul (Babati Mjini); Joseph Mkundi (Ukerewe) na Marwa Ryoba (Serengeti).

Kuondoka kwa wabunge hao, kumedaiwa na baadhi yao kuwa kumechangiwa na kile wanachodai, “kuwapo kwa migogoro kwenye vyama walivyokuwa.”

Mpaka sasa, wabunge saba wa Chadema na wawili wa CUF wameshahama vyama vyao na kujiunga na CCM.

Waliohama upinzani na kujiunga na CCM, ni pamoja na Julius Kalanga (Monduli); Dk. Godwin Mollel (Siha); Mwita Waitara (Ukonga), Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Kuchauka (Liwale).

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa barabara ya juu, Rais John Magufuli alinukuliwa akisema, wale wote ambao wamekabiliwa na mizigo kwenye vyama vyao, wanakaribishwa kujiunga na CCM.

Vyanzo vya taarifa kutoka ndani ya chama hicho vinasema, tangazo dhidi ya wapinzani, linalenga kuleta msukomo kwa baadhi ya waliopo mguu mmoja nje na mmoja ndani, kufanya haraka kuvihama vyama vyao na kujiunga na CCM.

“Kuna watu wako mguu ndani, mguu nje. Tangazo hili, linalenga kuwataka kufanya haraka kuondoka. Unajua kuna wabunge wa Chadema na CUF (Chama cha Wananchi), ambao tunawataka kujiunga na chama chetu na wengine wameomba wenyewe. Lakini kila tukiwafuatilia, wanaonekana kuwa na kigugumizi. Hawa ndiyo tunataka waondoke haraka,” anaeleza mmoja wa viongozi wa CCM aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini.

error: Content is protected !!