Saturday , 2 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kimenuka: Wabunge wengine Chadema, CUF mbioni kuondoka
Habari za SiasaTangulizi

Kimenuka: Wabunge wengine Chadema, CUF mbioni kuondoka

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love
TAKRIBANI wabunge tisa kutoka vyama viwili vikubwa vya upinzani bungeni – Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wako mbioni kuvihama vyama vyao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka kwa baadhi ya watu waliokaribu na wabunge hao zinasema, tayari wawakilishi hao wa wananchi, wamekamilisha majadiliano na baadhi ya viongozi wakuu wa vyama wanavyotarajia kujiunga navyo.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa MwanaHALISI ONLINE, hatua ya  kuondoka kwa wabunge hao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, kunatokana na kutoridhishwa kwao na kile wanachokiita, “ubinafsi” uliyopo kwenye vyama wanavyoondoka.

“Ni kweli kwamba kuna baadhi ya waheshimiwa wabunge, wataondoka kwenye vyama vyao muda wowote kabla ya kumalizika kwa mkutano huu wa Bunge la Bajeti,” ameeleza mtoa taarifa wetu ambaye hakupenda kutajwa gazetini.

Miongoni mwa wabunge wanaotajwa kuondoka sasa, baadhi yao ni wabunge wa Viti Maalum; ikiwa hilo litatendeka, hii itakuwa mara ya kwanza kwa wabunge wa aina hiyo, kufanya hivyo.

Anasema, “baadhi ya wanaohama, wameshakutana na mmoja wa viongozi wa Bunge kumuelezea mpango wao huo. Nimeelezwa kuwa naye ameridhia na amewatakia safari njema ya kisiasa huko wanakoelekea.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika kundi hili linalotarajiwa kuondoka, karibu wabunge sita wanaondoka Chadema na wanne wanatoka CUF.”

Katika orodha ya wabunge wanaotarajiwa kuondoka Chadema, mtoa taarifa anasema, watatu wamepanga kujiunga na NCCR- Mageuzi; mmoja ACT- Wazalendo na wawili wanaelekea CCM.

MwanaHALISI limepata orodha ya baadhi ya wabunge wanaotajwa kuondoka na kwamba wawili kati yao, mmoja anatokea Chadema na mwingine anatokea CUF. Wote wamethibitisha  kuwa wako njiani kutafuta maisha kwenye vyama vingine.

Kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja wiki tatu tokea mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu, kutangaza kuwa mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, amepanga kuondoka chama chake cha sasa na kujiunga na NCCR- Mageuzi.

Aidha, Komu ambaye alipata kuwa mkurugenzi wa fedha na utawala wa chama hicho, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuwa uamuzi wake wa kuondoka Chadema, umetokana na “chama hicho kuacha misingi yake ya kujenga demokarasia na kutafuta dola.”

Alitolea mfano wa matumizi mabaya ya rasimali za chama hicho, ikiwamo fedha zilizochangwa na wabunge wake kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, kwamba mamilioni hayo ya shilingi, yametumika kwa maslahi binafsi ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Chadema kilichangisha kwa kila mbunge kiasi fulani cha fedha kutoka kwenye mishahara yao ili kutunisha mfuko wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa rekedi zilizopo ofisi ya Bunge mjini Dodoma, kila mbunge wa Chadema anayetokana na Jimbo la uchaguzi, amechangishwa kiasi cha Sh. 520,000, huku wabunge wa Viti Maalum, wakipupukutishwa kiasi cha Sh. 1,560 000 kwa kila mwezi.

Kwa hesabu hizo, kama kila mbunge angetoa mchango wake kama ilivyopangwa, kulitarajiwa kukusanywa takribani kiasi cha Sh. 4.2 bilioni kwa muda wa miezi 56 ya uhai wa Bunge.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Komu alisema, takribani Sh. 3.4 bilioni, zilichukuliwa kutoka kwenye akaunti za Chadema na kutumika kwa matumizi mengine ambayo hayakupangwa.

Baadhi ya fedha hizo, zinadaiwa kuwa zilikopwa na mmoja wa viongozi wajuu ambaye aliziingiza kwenye mradi wa kilimo na kwamba baada ya mradi huo kushindwa kuleta faida, mhusika aliagiza hasara hiyo ibebe na chama.

Mbali na sakata hilo la fedha za michango ya wabunge, kingine ambacho baadhi ya wachambuzi wanakitaja kuwa sababisho la wabunge wa Chadema kuondoka, ni kuwapo kwa makundi ya uchaguzi wa ndani, majungu yanayopikwa na baadhi ya “marafiki wa Mbowe,” na chama kupoteza dira.

Kwa upande wa wabunge wa CUF, karibu wote wanaondoka wanafanya hivyo kutokana na kumeguka kwa chama hicho katika makundi mawili, kundi la Maalim Seif Sharif Hamad na Prof. Ibrahim Lipumba.

Katika orodha ya wabunge wa CUF, mmoja anatarajiwa kujiunga na ACT- Wazalendo, mmoja NCCR- Mageuzi na wengine CCM.

Mpaka sasa, wabunge tisa wa Chadema na wengine watano wa Chama cha Wananchi (CUF), wamevihama vyama hivyo ambavyo walivyovitumia kuingia bungeni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kurejea CCM.

Waliondoka Chadema na kujiunga na CCM, ni pamoja na mbunge wa Ukerewe mkoani Mwanza, Joseph Mkundi; mbunge wa Simanjiro, James Millya; mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul na mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Wengine, ni mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara; mbunge wa Siha, Godwin Molleli; mbunge wa Monduli, Julius Kalanga na mbunge wa Serengeti, mkoani Mara, Mwalimu Ryoba Chacha.

Kwa upande wa CUF, waliondoka ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Ahmed Katani (Tandahimba), Zuberi Kuchauka (Liwale), Abdallah Mtolea (Temeke), Ahmed Juma Ngwali (Wawi) na Juma Hamad Omari (Ole).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Mwalimu jela miaka mitatu kwa rushwa

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi, wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu...

Habari za Siasa

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua programu ya...

Habari za Siasa

AG aiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia mawakili wanaokiuka maadili

Spread the loveMWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Eliezer Feleshi, ameagiza Kamati...

Habari za Siasa

Jaji avunja ukimya sakata la Mpoki kusimamishwa uwakili

Spread the loveJAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amekitaka Chama cha...

error: Content is protected !!