October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge watoa kilio hamahama watumishi wa X-Ray, Spika atoa maagizo

Spread the love

 

WABUNGE Francis Ndulane (Kilwa Kaskazini) na Minza Mjika (Viti Maalum) wamefikisha bungeni kilio cha hama hama ya watumishi wa kipimo cha uchunguzi wa afya ya binadamu (X-Rays), wakihoji lini Serikali itapeleka watumishi ili kuziba mapengo yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Wabunge hao wametoa kilio hicho leo Ijumaa, tarehe 10 Juni 2022, katika kipindi cha maswali na majibu, bungeni jijini Dodoma.

Akifikisha kilio hicho, Minza amesema Hospitali ya Wilaya ya Meatu ndani ya miaka 30, imekuwa inakabiliwa na changamoto ya hama hama ya watumishi wa X-Ray na kuhoji lini Serikali itapeleka mtumishi wa kudumu.

“Nilitaka kujua lini mtaalamu ataletwa sababu tatizo hili limekuwa la muda mrefu sana. Leo Wilaya ya Meatu Hospitali ina zaidi ya miaka 30 lakini hatujawahi kupata mtumishi wa kudumu wa X-Ray,” amesema Minza.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Festo Dugange, amejibu swali hilo akisema katika mwaka wa fedha wa 2021/22, Serikali ilitoa ajira za watumishi wa kada ya afya 7,612, ikiwemo watalaamu wa X-Ray na kwamba Julai, 2022 watapelekwa katika vituo vyao vya kazi, ikiwemo kwenye Hospitali ya Wilaya ya Meatu.

Kwa upande wake, Ndulane amesema katika Hospitali ya Kipatimu kulikuwa na mtumishi wa X-Ray, aliyefanya kazi kwa muda wa miezi sita, kisha akahamishwa bila ya Serikali kuziba pengo lake.

Dk. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Tanzania

“Oktoba 2021, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitembelea jImbo la Kilwa Kaskazini na alifika katika Hospitali ya Kipatimu akakuta kuna changamoto kubwa ya mtumishi wa X-Ray, baada ya kuwa X-Ray ilinunuliwa miaka zaidi ya minne ikiwa haitumiki kwa kukosa mtumishi,” amesema Ndulane na kuongeza:

“Swali ni kwamba, mtumishi aliletwa akakaa miezi sita, lakini juzi juzi hapa ameondolewa. Nataka kujua Serikali ina mpango gani wa kumrejesha mtumishi aliyeondoelewa juzi juzi?”

Dk. Dugange alimjibu Ndulane akisema “ni kweli kwamba tulipeleka mtumishi Hospitali ya Kipatimu, lakini kwa sababu za kiutumishi amehamishwa, lakini kwenye ajira hizi ambazo watumishi watapelekwa Julai, tayari amepangwa mtumishi wa X-Ray kwenye Hospitali ya Kipatimu.”

Licha ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameishauri Serikali ihakikishe inapeleka mtumishi wa afya kabla ya kumhamisha mtumishi katika hospitali husika, ili kuepusha changamoto hiyo.

“Serikalini mna utaratibu wenu, lakini huu sio utaratibu mzuri wa mtumishi kuwepo watu wakawa wanapata huduma, halafu anaondolewa kabla mtumishi mwingine hajapelekwa hapo. Kwa sababu watu watakuwa wanaenda kuhudumiwa na nani?” amesema Spika Tulia na kuongeza:

“Mlivyompeleka mwanzo alianza kazi, mnavyomuondoa mhakikishe mwingine ameshaenda pale. Nadhani ni utaratibu mzuri.”

error: Content is protected !!