July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge watilia shaka bajeti

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akisoma bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16

Spread the love

BAADHI ya wabunge wameikosoa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16 ambayo imewasilishwa bungeni leo na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya. Anaandika Jimmy Mfuru … (endelea).

Wengi wao wamesema kwa kuisikiliza bajeti iliyotangazwa ni nzuri, shida kubwa ni kama itatekelezwa ipasavyo. Hofu yao inatokana na walichoita kama uzoefu wa mwenendo wa serikali kuvuruga bajeti kwa utekelezaji usio  na tija kwa wananchi.

Tatizo kubwa lililotajwa kama changamoto ni mtindo wa serikali kutumia visivyo fedha zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vile mradi wa kusambaza umeme vijijini.

Esther Bulaya, mbunge wa Viti Maalum (CCM), amekuwa mchungu kwa kutumia eneo hilo kuibana serikali akisema katika bajeti ya mwaka unaokwisha, ilitumia fedha hizo kwa mambo mengine na hivyo kuzorotesha utekelezaji wa miradi hiyo inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Wakati wa kujadili makadirio ya bajeti ya Wizara na Nishati na Madini, Bulaya alizuia mshahara wa waziri akitaka serikali itoe tamko itamchukulia hatua gani kiongozi aliyeidhinisha matumizi kinyume na Bunge lilivyopitisha.

Bulaya pia amekosoa ongezeko la tozo kwa mafuta ya petroli akisema litaongeza gharama kwa watu wa chini, ikiwemo kulazimika kulipa zaidi kwa ajili ya nauli za usafiri nchini.

Serikali imetangaza tozo mpya ya Sh.100 kwa mafuta ya dizeli kutoka Sh. 50 kwa lita, huku mafuta ya taa yakiongezwa tozo kufikia Sh.150 kutoka Sh.50. Hoja ya serikali ni kudhibiti uchakachuaji wa mafuta.

Amesema utamaduni wa serikali kuendelea kukopa bila uangalifu umezidisha mzigo kwa wananchi kwani deni la taifa limekua kwa asilimia 20 kufikia Sh. 35 trilioni ndani ya mwaka mmoja.

“Inasikitisha serikali haijatilia mkazo kwenye jukumu la kutafuta vyanzo vipya na vya uhakika vya mapato na hivyo kujilemaza kutegemea mikopo,” amesema Bulaya ambaye pia ni mwandishi wa habari.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amesema utamaduni wa serikali kuivuruga bajeti kwa vile ilivyopitishwa na Bunge unaisababisha kushindwa kuwa adilifu katika kutekeleza mipango yake.

Hiyo ndiyo amesema imechangia kuiweka serikali pabaya kwa kutekeleza bajeti yake kwa nusu tu ya matarajio.

Mdee amesema inakuwa vigumu kuamini kama itatekelezeka kwani hata hizo tozo za kwenye mafuta huenda zisipelekwe zote REA kama ilivyofanyika katika bajeti ya mwaka unaomalizika ambapo zilipelekwa asilimia 50 tu.

Zarina Madabida, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), amesifu bajeti akisema haikuongeza kodi kwenye vinywaji vikali, soda na sigara, hatua iliyo tofauti na desturi kwa serikali kutumia bidhaa hizo kila mwaka kupandisha kodi zake.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema serikali haijawahi kuwa na ubunifu wa kupata vyanzo vipya vya mapato.

“Kwanza mimi sijaielewa hii bajeti na hivyo sina la kusema kwa kuwa bajeti ni ileile, watu walewale, serikali ileile… hakuna jambo jipya hapa.”

“Unajua serikali hii imechoka haina jambo lolote jipya na hakuna mtu mwenye mawazo mapya ya kubuni vyanzo vipya vya mapato. Kama wangekuwa wabunifu, hata kodi za majengo zingeweza kuliingizia taifa pato kubwa,” amesema Lissu.

Augustine Mrema (Vunjo, TLP) amesema hajaona kitu kipya katika bajeti mpya kwani “Ni bora wangekaa wenyewe wakaipitisha, sisi (wabunge) tukabaki nyumbani, kwa sababu kila tunachopitisha hakitekelezeki.”

Amesema kila mwaka bunge linapitisha bajeti na fedha za miradi ya maendeleo zinatengwa, lakini ni “hewa hakuna kinachotekelezeka.”

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) ameibeza bajeti akisema haina jambo lolote jipya. “Serikali haikuwa na sababu ya kuongeza tozo ya mafuta… ilikuwa na uwezo wa kutafuta vyanzo vingine vya mapato.”

Mpina ambaye amechukua fomu ya CCM kutafuta uteuzi ili kugombea urais, amesikitika kwamba serikali inaahidi kupeleka fedha kwenye miradi ya umeme vijijini ilhali inaonesha inakiuka mpango wake yenyewe.

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), ameisifia bajeti akisema serikali imeonesha utashi wa kutaka kujitegemea badala ya kuendelea kutegemea wafadhili kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.

Cheyo amesema iwapo pesa zinazopatikana kwenye tozo ya mafuta zitapelekwa katika miradi ya umeme vijijini kama ilivyoahidiwa, serikali itajenga uwezo wa kujitegemea. “Katika eneo hili Watanzania watapata huduma ya nishati ya umeme kwa urahisi,” amesema.

error: Content is protected !!