August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge watano wa jiji hawa hapa

Spread the love

HATIMAYE wabunge watano (5) watakaoingia katika baraza la madiwani la halmashauri ya jiji la Dar es Salaam wamepatikana, anaandika Kondo Tutindaga.

Wabunge waliochaguliwa kuingia katika baraza la jiji, ni Halima Mdee (Kawe), Saed Kubenea (Ubungo), Abdallah Mtolea (Temeke), Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni) na Mussa Azzan Zungu (Ilala).

Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepata nafasi mbili, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata nafasi mbili na Chama cha Wananchi (CUF), kimepata nafasi moja.

Jiji la Dar es Salaam lina majimbo 10 ya uchaguzi, ambapo CCM ina wabunge wa wanne na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umenyakua viti sita. Sheria inayounda jiji la Dar es Salaam, inatambua wabunge watano tu kuwa wajumbe wa baraza la madiwani; kati ya wajumbe hao, angalau mmoja awe mwanamke.

Akiongea na MwanaHALISI Online, Mdee amesema, mgawanyo huo umezingatia matakwa ya kisheria ya kila halmashauri kuwa na mwakilishi. Amesema kwa sasa, jiji la Dar es Salaa lina halmashauri tano – Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo na Ilala.

“Tumeona tufanye makubaliano kwamba kila chama kipate uwakilishi badala ya utaratibu wa kupiga kura. Hii imetokana na utata uliopo kwenye sheria nzima inayounda jiji,” ameeleza.

Amesema, katika makubaliano hayo, CCM wamepata viti viwili na UKAWA tumepata viti vitatu.

Naye Kubenea akizungumzia uchaguzi huo alisema, “yale yalikuwa maridhiano yenye tija kwa pande zote. Kuna utata mkubwa wa kisheria na hivyo tumeona ili kumaliza suala hili, tufanye makubaliano kwa kuwa bila hivyo, shughuli za jiji zilikuwa zimekwama.”

Amesema, “baraza lisingeweza kuitwa bila kuwapo uwakilishi wa wabunge. Miradi na rasimali za jiji zilikuwa zinaendelea kuporwa na wajanja kwa kuwa baraza la madiwani haliwezi kufanya shughuli zake.

“Uchaguzi wa Naibu Meya umekwama kwa kuwa wabunge hawajakubaliana kuhusu uwakilishi wao katika jiji. Hivyo, kwa kuzingatia yote hayo, tukaona ni muhimu kufanya maamuzi haya mapema ili shughuli za jiji ziendelee.”

Kwa mujibu wa Kubenea, kulikuwa na uwezekano   UKAWA kuingiza wajumbe wanne kati ya watano waliohitajika, lakini kutokana na kuona jambo hilo litawapotezea muda na lingeweza kutumika kuvunja uongozi wa jiji, wakakubaliana wenzao wa CCM kugawana viti.

Uchaguzi wa Naibu Meya wa jiji umepangwa kufanyika leo, Alhamisi saa tano asubuhi katika ukumbi wa Karimjee.

error: Content is protected !!