July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge wataka Yanga SC iitwe bungeni, Spika ang’aka

Spread the love

 

BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamemtaka Spika Dk. Tulia Ackson aruhusu Klabu ya Yanga SC. ambayo wametwaa ubingwa wa 28 wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka huu, watinge ndani ya ukumbi wa Bunge.

Shinikizo hilo limetolewa leo tarehe 16 Juni, 2022 baada ya Timu ya Taifa ya Soka la Walemavu (Tembo Warriors) kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge heshima ambayo pia ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Timu ya Taifa wasichana ya chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kwa mara ya kwanza tarehe 7 Juni, 2022 Bunge lilitengua kanuni ya 160 (1) ambayo inatoa masharti kwa wageni wasio wabunge kuingia ndani ya ukumbi na kuiwezesha Serengeti Girls kuingia mjengoni na kukalia viti vya wabunge.

Aidha, baada ya Spika Tulia kutoa pongezi kwa Tembo Warriors kwa kutinga katika faina ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika nchini Uturuki Septemba na Oktoba mwaka huu, pia aliahidi kila timu yoyote ya Taifa itakayotinga fainali ya mashindano ya kombe la dunia itaitwa ndani ya ukumbi wa Bunge.

“Tutafanya hivi kwa kila timu itakayofuzu kucheza kombe la dunia, tunawatakia kilala kheri, Twiga Stars, Taifa Stars, timu za Netball, nimesema timu za Taifa tusije kuchanganya mambo hapa, naona watu wa Yanga wanataka Yanga aingie humu ndani,” amesisitiza Spika Tulia.

Licha ya baadhi ya Wabunge kupiga kelele Yanga nayo iingie ndani ya ukumbi huo, Spika Tulia alirudia kwa msisitizo kuwa heshima hiyo ni kwa timu za Taifa pekee.

Awali Spika Tulia amesema ili kuweka usawa nchini lakini pia kutoa morali kwa wachezaji wote wa timu yoyote nyingine itakayofuzu kucheza kombe la dunia italetwa hapa bungeni ili waipe baraka zao kwenda huko.

“Kwa hiyo hata timu nyingi zisijione wanyonge hivi hapana! zikae mkao sawa tu Bunge tupo tayari kutoa morali ya namna hii ya watu kuja kukalia viti vya waheshimiwa wabunge na wao ni waheshimiwa wabunge kwa muda kwa majina yao,” amesema Spika Tulia.

Amesema Watanzania wanawatazama na kuwategemea Tembo Warriors kwamba walivyofanya vizuri ngazi hii watafanya vizuri zaidi ngazi inayofuata.

“Na kuingia kwenu hapa ni ahadi kuwa Kombe mtarudi nalo kwa hiyo tunawatakia kilala kheri katka michezo iliyo mbele yenu.

“Kama mnavyofahamu nchi nzima inasema Rais Samia anaupiga mwingi na sisi wabunge tunajua Rais anaupiga mwingi, sasa muende na nyie huko kwenye kombe la dunia mkawaoneshe Tanzania kuna Rais anayeupiga mwingi,” amesema Spika Tulia.

error: Content is protected !!