Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge wamchambua Dk. Mpango, wampongeza Rais Samia
Habari za Siasa

Wabunge wamchambua Dk. Mpango, wampongeza Rais Samia

Waziri Mkuu akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Spread the love

 

WABUNGE wa Tanania wamemchambua Dk. Philip Mpango (63), kuwa ni mtu sahihi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dodoma…(endelea).

Baadhi ya wabunge hao wakiongozwa na mawaziri Profesa Joyce Ndalichako wa elimu; Profesa Palamagamba Kabudi (wa mambo ya nje), Willium Lukuvi wa Ardhi na Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima na mbunge wa Geita, Joseph Msukuma wamesema “Mpango ni mtu sahihi.”

Wamemchambua Dk. Mpango, wakati wakizungumzia mapandekezo yaliyowasilishwa bungeni leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021, jijini Dodoma na mpambe wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia amempendekeza Dk. Mpango ili kuchukua nafasi yake baada ya yeye (Samia), kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi 2021.

Ni baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021, Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam na mwili wake, kuzikwa 26 Machi 2021, nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Dk. Phillip Mpango, Makamu wa Rais Tanzania

Aliyekuwa wa kwanza kuchangia hoja hiyo ni; Profesa Ndalichako akisema “mimi nina bahati ya kumfahamu Dk. Mpango, chuo kikuu alikuwa ni mchapa kazi, alikuwa anasimamia vyema kazi zake na alikuwa analea sana vipawa vya wachumi na nina mfahamu kama mcha Mungu na katika maisha yake.”

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema, “Dk. Mpango anaipenda sana nchi yake, mtu mwenye uchungu na Taifa zake, anayetamani kuona nchi inasonga mbele na mtakubaliana na mimi, ni watu wachache sana wanadumu kwenye nafasi ya wizara ya fedha, amekaa kwa zaidi ya miaka mitano.”

“Dk. Mpango huwa hacheki na watu ambao wanachezea chezea rasilimali za nchi na mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, ametuletea jina sahihi hasa kutokana na Dk. Mpango kuwa mtu sahihi kabisa na sisi tumpitishie hili jina.”

“Atakwenda kuwa kiungo mzuri katika kusimamia rasilimali za Taifa na kuwawezesha wananchi wanyonge iweze kusonga mbele zaidi kwani uchumi na mapato ya serikali na tumuunge Mama yetu, Rais Samia kwa kumpitishia jina la Mpango,” amesema Profesa Ndalichako ambaye pia ni mbunge wa Kasulu Mjini.

Naye Profesa Kabudi ameanza kwa kusema “leo ndiyo siku aliyoifanya bwana. Tumpongeza Rais wetu, Samia Suluhu Hassan toka kutokea kwa msiba, ametuongoza vizuri sana. Ametuletea jina sahihi ambalo hakika, anasitahiki kuwa makamu wa Rais, Philip Mpango.”

Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

“Mambo haya hupanga Mungu na Mungu akiyapanga hutimia. Tunampongeza Rais kwa kukuteua wewe (Dk. Mpango) kuwa msaidizi wake. Philip una sifa zote. Ulifiwa na baba yako akiwa mdogo, ukatunzwa na mama yako na watoto wanaofiwa na baba zao, huwapandisha zaidi.”

Profesa Kabudi amesema “naamini Mungu amemuangaza mama Samia Suluhu Hassan, kukuteua wewe kuwa makamu wa Rais. Niwaambie Watanzania, Philip Mpango amejaaliwa unyenyekevu, upole lakini uthabiti na amejaaliwa kauli ambazo hazibadiliki.”

“Taifa hili limemwandaa vizuri toka utawala wa Jakaya Kikwete na ana uzoefu katika nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizara ngumu ya fedha na mipango ikiwemo kuingia katika uchumi wa kati,” amesema Profesa Kabudi.

Waziri Lukuvi amesema “namfahamu Mpango tangu alipoingia madarakani. Kwa mtu mwenye akili timamu, kugombana na Mpango huwezi kusikia. Dk. Mpango ni mtu sahihi kabisa kwani ni mtu anayefaa, ana stahili na Dk. Mpango ni mcha Mungu sana.”

“Ukifika nyumbani kwake, utapokelewa na ishara za ucha Mungu. Hata alipoumwa alimtanguliza Mungu mbele. Tunamshukuru Rais Samia kwa kumwona na tunamhakikishia tutampa ushirikiano wa kutosha. Huyu ni mwenzetu humu kama miaka sita na amesimamia kutafuta fedha ili kutekeleza miradi iliyoahidiwa na serikali,” amesema Lukuvi

“Tunakuombea uendelee kuwa Dk. Mpango huyu huyu na si vinginevyo,” amesema.

Kwa upande wake, Askofu Gwajima amesema “jicho lililomwone makamu wa rais aliyeteuliwa ni jicho kubwa kuliko sisi, jicho lililomwona zaidi ya Watanzania mamilioni la Mama Samia, ni jicho kubwa sana.”

Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe

“Mama Samia yuko mawinguni, yuko juu sana na kwa sababu yeye yuko juu, ndiyo maana kwa jicho lake, amempata Philip Mpango ili awe makamu wa Rais.”

Naye Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Joseph Msukuma amesema “dalili ya mvua ni mawingu, naona mama Samia atatuvusha. Kusema ukweli huyu Dk. Mpango ni waziri ambaye hana makundi na huu ni mfano kwa mawaziri wengine. Anamsikiliza kila mtu kama waziri na mimi siku moja nilimwomba lifiti akanipa.”

“Kuna mawaziri wengine, wakiingia kwenye ma V8 hawakujui, huu ni mfano kwa wengine na hakuna anayekunyima kura,” amesema Msukuma anyejiita yeye ni kiongozi wa wabunge wenye elimu ya darasa la saba.

“Dk. Mpango unakwenda kuwa mshauri namba moja wa Rais, mweleze Rais hali ya wananchi wanyonge, umekuwa humu ndani, umetusaidia kama taifa, kutoka uchumi wa chini hadi wa kati, kuna changamoto kadhaa kama kwenye madini, unajua ulikuwa TRA, sasa umepewa rungu kubwa.”

“Matatizo ya TRA unayajua, kuna vitu vinawafanya wafanyabiashara kuwa na tatizo. Hakuna mtu anayekataa kulipa kodi. Kila la kheri sana Mpango,” amesema Msukuma

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!