October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge waliofukuzwa CUF na kupoteza ubunge washinda kesi

Wabunge wa CUF waliovuliwa uanachama wakiwa mahakamani wakisikiliza shauri lao la kupinga hatua hiyo

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania leo tarehe 12 Agosti, 2022, imesoma Hukumu ya Kesi namba 143 ya Mwaka 2017 iliyofunguliwa na Miza Bakari Haji na wenzake 9 dhidi ya CUF, Spika wa Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Manispaa za Ubungo na Temeke wakipinga kufukuzwa uanachama na hatimaye Ubunge na Udiwani wa Viti Maalum kupitia CUF. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Dk. Juliana Masabo Mahakama Kuu imetamka kwamba CUF ilivunja Katiba yake na ilivunja haki za wadai kwa kuwafukuza uanachama bila kuwapa nafasi ya kusikilizwa.

Pia imesema CUF iliwavua uanachama kabla mchakato wa Rufaa zao walizokata kupinga kufukuzwa uanachama kuwa zimesikilizwa ndani ya chama.

Mahakama imesema imezingatia ushahidi kadhaa, ikiwemo kukiri kwa CUF yenyewe katika utetezi wake kuhusu mambo kadhaa, ikiwemo haki ya Kikatiba ya kukata Rufaa.

Hata hivyo Mahakama Kuu imetamka kwamba Spika na Tume ya Uchaguzi hawana hatia kwani wao walipokea tu taarifa kutoka CUF kuhusiana na wadai kufukuzwa uanachama wao.

Mahakama pia imetamka kwamba kila upande utabeba gharama zake za kuendesha shauri husika.
Itakumbukwa kuwa Julai 25, 2017 Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alitangaza kuwafuta uanachama Wabunge wanane na Madiwani wawili kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kinidhamu, kukihujumu chama, kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Wabunge na madiwani hao walifukuzwa baada ya kuibuka kwa mgogoro mkubwa ndani ya chama hicho iuliosababisha mpasuko uliosababisha Katibu Mkuu wa Chama hicho hayati Maalim Seif Sharif Hamad kuondoka na wafuasi wake kuhamia chama Cha ACT-Wazalendo.

Chanzo cha mgogoro huo kilisababishwa na kurejea kwa Lipumba baada ya kuwa alijiuzulu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 akipinga Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumsimamisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais.

Waliovuliwa ubunge ni Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohemed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally al Kassmy na Halima Ali Mohamed.

Julai 26, 2017 taarifa kutoka ofisi ya Bunge ilieleza kuwa Spika Job Ndugai ameridhia kufutwa uanachama kwa Wabunge hao na hivyo nafasi zao ziko wazi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Spika Ndugai alisema amejiridhisha kuwa Wabunge hao wamefutiwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo hawana sifa za kuendelea na Ubunge.
Spika alitangaza nafasi hizo kuwa wazi na kumuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa Sheria.

error: Content is protected !!