January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge waivaa Serikali hatima ya ‘Bureau de change’

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamadi Masauni

Spread the love

 

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamadi Masauni imetoa wito kwa wafanyabiashara wa maduka ya kubadilisha fedha nchini ‘Bureau de change’ ambayo yalifungwa na Serikali, waende kuchukua vifaa vyao vilivyochukuliwa na kikosi kazi kilichokuwa katika operesheni hiyo. Anaripoti Hellena Mkonyi, TUDARCo … (endelea).

Masauni ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Septemba bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge wanne wa CCM ambao kwa nyakati tofauti walihoji hatima ya wafanyabiashara wa maduka hao.

Alikuwa ni Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo (CCM) ambaye aliuliza swali la msingi kwamba nini hatma ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha nchini ‘Bureau de change’ yaliyofungwa na Serikali nchini kote.

Tarimo amesema ukaguzi uliofanyika mwaka 2018/19 ulipelekea maduka mengi ya kubadilisha fedha za kigeni kufungwa kutokana na kubainika kuendesha biashara bila kuzingatia sheria na kanuni husika.

Mbunge huyo amesema vigezo na masharti yaliyowekwa na Serikali kwamba lazima mmiliki wa duka kuwa na mtaji kuanzia milioni 300 hadi bilioni moja ni kiwango kikubwa ambacho kinafifisha uwekezaji kwenye sekta hiyo.

Akijibu swali hilo, Masauni amesema kwa ujumla, hali ya upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ni ya kuridhisha.

“Maduka yaliyofungwa pamoja na makampuni mengi yanayotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini, yanaruhusiwa kuomba leseni Benki Kuu kwa kuzingatia matakwa ya sheria za fedha za kigeni ya mwaka 1992 na kanuni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ya mwaka 2019.

“Hadi kufikia tarehe 30 Julai 2021, Benki Kuu ilikua imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakuwa wamekidhi vigezo,” amesema.

Aidha, Masauni amesema hatima ya vifaa vilivyochukuliwa ni kwamba wafanyabiashara waliitwa na kufanya majadiliano kisha waliopaswa kulipwa walilipwa na vifaa vya vilirejeshwa.

Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini (CCM)

“Wale ambao wanapaswa kuchukua vifaa vya waende kuchukua hii ni kauli ya serikali kama ambavyo majadiliano yalifanyika basi waende kuchukua na kama kuna mapungufu yoyote tunaweza kufanyia kazi,” amesema.

Aidha, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe N’genda, Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo na Mbunge Simanjiro, Christopher Olesendeka nao pia waliiibana serikali kuhusu hatima ya suala hilo na kudai kuwa kulitumika nguvu kubwa kupitia kikosi kazi kisichokuwa na utaalam wa mambo ya kodi.

Akijibu hoja hizo Masauni amesema kwa kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haitaki kodi ya dhuluma, hivyo wafanyabiashara wanaitwa kwenda kuchukua vifaa vyao.

Amesema wale ambao hawakuridhika na tathmini iliyofanywa na kikosi kazi hicho wanaweza kukata rufaa.

Pia amesema kikosi kazi kilichofanya operesheni hiyo ni kitengo maalumu cha uchunguzi – TRA hivyo sio kweli kwamba si kitengo kinachozingatua taaluma.

error: Content is protected !!