May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge waisusia ofisi ya Samia Suluhu

Luhaga Mpina Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira

Spread the love

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imetangaza kutoshirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mazingira kama ofisi hiyo haitakuwa tayari kufanya ziara katika maeneo ya migodi na maeneo ya mabonde, anaandika Dany Tibason.

Wabunge wa kamati hiyo, waligoma kujadili taarifa ya utupaji wa taka katika migodi iliyowasilishwa na Luhanga Mpina, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kile walichosema kuwa ni mapungufu makubwa pamoja na upotoshaji uliopo katika taarifa hiyo.

“Wabunge hatupo kwa ajili ya kufanya kazi za serikali wala kuwafurahisha mawaziri na timu yako, Tupo kwa ajili ya kuisimamia serikali kwa masilahi ya wananchi,” amesema Tauhida Nyimbo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM).

Tauhida amehoji na kusema, “Hivi Naibu Waziri (Mpina) na timu yako, mnatuletea hii taarifa tujadili. tujadili kitu gani au nyie hamjui wajibu wenu mnadhani sisi ni wasaidizi wenu au tunafanya kazi za serikali?”

Khatibu Haji Kombo (CUF), Mbunge wa Konde, amesema, “Unatuletea taarifa iliyojaa mapicha mengi na kutuelezea mambo ambayo hatuyajui na mmetunyima fursa ya kufanya ziara ya kujirishisha na taarifa zenu. Nendeni na taarifa yenu hatuwezi kuijadili hadi tufanye ziara ili kujiridhisha na kilichoandikwa.”

Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema), aliunga mkono kufukuzwa kwa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na kusema kuijadili taarifa hiyo ni kutowatendea haki wananchi.

“Taarifa inayohusu taka sumu katika migodi si sawa na kusoma kitabu cha hadithi au gazeti kwani ukiwa unasoma vitabu vitu hivyo huwezi kuhoji. Tunataka tujionee hali halisi kuhusu taka na sumu katika migodi ikiwemo zile zinazoathiri vyanzo vya maji,” amesema.

Vicky Kamata, makamu mwenyekiti wa kamati hiyo akiongoza kikao hicho amesema, “Hatuwezi kupitisha ripoti hii, kama serikali haina fedha za kupeleka wabunge katika maeneo yenye matatizo wakakague basi ifute kabisa kamati hiyo.”

error: Content is protected !!