August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge waishambulia Sumatra

Jengo la Bunge la Tanzania mjini Dodoma

Spread the love

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba leo wamegomea mapendekezo ya marekebishi ya Sheria ya Sumatra sura 413 na Sheria ya Leseni za Usafirishaji sura 317, yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Uthibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), anaandika Dany Tibason.

Wajumbe hao wakichangia katika kamati hiyo wamesema Sumatra haina malengo ya dhati ya kukabiliana na uthibiti wa ajali, badala yake wamekuwa wakielekeza nguvu kwa lengo la kukusanya maduhuri ya serikali.

Akichangia hoja zilizowasilishwa na Sumatra, Olemeiseyeki Gibson, Mbunge wa Arumeru Magharibi (Chadema) amesema, katika taarifa iliyowasilishwa na Sumatra inalenga zaidi katika ukusanayaji wa mapato kwa kupendekeza kuwepo kwa faini kubwa badala ya kupambana na kudhibiti ajali.

Amesema katika mapendekezo ya marekebisho ya sheria, inaonesha ni jinsi gani Sumatra walivyojipanga kukabiliana na mmiliki wa chomba cha usafiri badala ya kupambana na dereva ambaye wakati mwingine anaweza kusababisha ajali kwa uzembe.

Mbunge huyo amesema anaishangaa Sumatra kuona kuwa na mapendekezo ya utozaji wa adhabu kwa ajili ya ufifishaji wa makosa ambapo hapo awali ilikuwa kati ya Sh.10,000 hadi Sh. 50,000 na kuwa kati ya Sh. 200,000 hadi Sh. 500,000.

Amesema hatua hiyo haiwezi kupunguza ajali za barabarani na badala yake kinachotakiwa ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ikiwa ni pamoja na kujitanua katika maeneo mbalimbali badala ya kutumia nafasi ya kukamata na kutoza fedha.

Mohameid Mchagerwa, mwenyekiti wa kamati hiyo amesema taarifa ya mapendekezo ya Sumatra kubadilisha sheria waliyohitaja haina mashiko kwani ina upungufu mkubwa.

Kutokana na hali hiyo ameisema kamati haiwezi kukubaliana na maombi ya Sumatra kwa kuomba kubadilisha sheria na badala yake wanatakiwa kupitia maombi yao upya ili waweze kuona namna ya kuondokana na fikra za kuongeza adhabu ya faini kubwa badala ya kutoa elimu kwa Umma.

Lakini pia wametakiwa kufikiria namna ya kuweka utaratibu wa kumwajibisha dereva ambaye atasababisha uzembe badala ya kumtwisha mzigo mmiliki wa chombop cha usafirishaji.

Akiwasilisha katika kamati hiyo Gillard Ngewe, Mkurugenzi wa Sumatra amesema ili kuweza kupunguza ajali nchini, aliiomba Kamati ya Bunge kubariki mapendekezo yao.

error: Content is protected !!