Sunday , 25 February 2024
Home Habari Mchanganyiko Wabunge waichambua Bajeti
Habari Mchanganyiko

Wabunge waichambua Bajeti

Bunge likiendelea na vikao vyake
Spread the love

BAADHI ya Wabunge wamesema kitendo cha Bajeti ya Serikali kuondoa kodi kwenye mabango na ushuru wa mazao kinalenga kufifisha shughuli za maendeleo kwenye halmashauri za mijini na vijijini huku wengine wakipongeza na kusema ni bajeti bora, anaandika Dany Tibason.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online kwa nyakati tofauti mjini Dodoma leo, wamesema ni bajeti yenye takwimu zaidi na kwamba haina unafuu kwa maisha ya watanzania.

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo  (Chadema), amesema baadhi ya maeneo kwenye bajeti ni mazuri lakini wameshindwa kutengeneza utaratibu wa kuyafanya yawe mazuri zaidi.

Amesema kuondoa ada ya magari (Road License) ni jambo zuri lakini kuongeza gaharama za mafuta ni kuwaumiza watanzania wote, gharama za maisha na huduma zitakuwa juu.

“Bado bajeti hii ni tegemezi kwa sababu inaonekana kuna kuhitaji misaada na deni la taifa linaonekana kuongezeka…kuondoa kodi ya mabango, serikali inalenga kuziumiza halmashauri zinazoongozwa na wapinzani maana nyingi zitakosa mapato na shughuli nyingi za maendeleo zitakwama,” amesema Kubenea.

Naye William Ngeleja, Mbunge wa Sengerema  amesema bajeti ni nzuri, serikali imekuwa ikizingatia maslahi ya wananchi ingawa wapo watu wanaosema gharama za maisha zitapanda kwa kuongeza kodi ya sh. 40 kwenye mafuta sio kweli.

“Ilikuwa ukienda TRA leo wanakutoza kodi hata kwa magari yaliyokuwa yamepaki muda mrefu, sasa hivi itakuwa inatozwa kwenye magari yanayotembea na wanaomiliki magari ni wale wenye daraja la kati la uchumi.

“Bajeti hii inasema inatoa unafuu kwa vifaa vinavyokuja kuweka msingi wa ujenzi wa viwanda kiuhalisia sio rahisi sana kufanya bajeti itakayokidhi matarajio lakini kwa hii naiona ni bajeti ya wananchi,” amesema Ngeleja.

Amina Molle, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), amesema sio rahisi kwa bajeti kumridhisha kila mwananchi huku akipongeza kitendo cha serikali kuondoa kabisa kodi kwenye vifaa vya wenye ulemavu.

“Bajeti inaandaliwa na wanadamu wapo watakaosema haijawaridhisha lakini kwangu naiona ni bajeti bora imezingatia mambo mengi hasa hili la walemavu ni zuri sana maana ndio kilio chao siku zote,” alisema Mollel.

Kasuku Bilango, Mbunge wa Buyungu  (Chadema), amesema bajeti hiyo ni changa la macho kwa kuwa imejaa takwimu na haina uhalisia kwa sababu pesa za maendeleo haziendi zote na kwa wakati huku akilaumu mazoea ya serikali kutafuta mapato kwenye sigara na pombe.

James Mbatia, Mbunge wa Vunjo  (NCCR-Mageuzi) amesema bajeti haina mwelekeo wa kumsaidia mwananchi wa kawaida kwa kuwa ni tegemezi kwa asilimia 37 hivyo haitekelezeki.

“…Hii ni bajeti ya kisiasa, kuongeza ushuru wa mafuta ni kuwatesa wananchi yaani serikali badala ya kuhimiza kodi inafuta kodi maana yake makusanyo yatakuwa finyu, hakuna maendeleo,” amesema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.

Kangi Lugora, Mbunge wa Mwibara  amesema bajeti ni nzuri kwa kuwa inamgusa mtu wa hali ya chini na wakulima ni bajeti ya kwanza nzuri.

“Kuna vitu vingine wabunge tunatakiwa kuvijadili, hatuwezi kuendelea kutafuta kodi kwenye bpombe na sigara wakati kuna vyanzo vingi vya mapato huu ni uzembe wa serikali,” amesisitiza.

Suzan Kiwanga, Mbunge wa Mlimba  (Chadema) amesema kuondolewa kwa ada ya magari wengi wamefurahia lakini hawakujua athari zake kwa kuwa kodi ya mafuta inawaumiza wananchi wote katika sekta mbalimbali.

“Bei za usafirishaji zitaongezeka tutegemee gharama za maisha zitaongezeka, unaposema unapunguza ushuru kwenye halamshauri kutamsaidia mfanyabaishara sio mkulima kwa hiyo ile dhana ya serikali kwamba 2020 kila halmashauri ijitegemee kwa angalau asilimia 25 haitawezekana kwa hiyo hii ni pigo kwa halmashauri mbalimbali.

“Lakini kibaya zaidi tunapoenda kutimiza malengo yetu Tamisemi inatoa matamko tutenge sh. milioni 30 za mwenge tutazitoa wapi wakati zimepunguziwa uwezo wa kukusanya huku ni kutuvuruga, bajeti ni ngumu tutegemee maisha magumu sana kwa bajeti hii,” amesisitiza Kiwanga.

Salma Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum  (CUF) amesema kuondoa kodi ya mafuta ya kupikia, vyakula vya mifugo japo kidogo ndiyo inayomfikia mwananchi wa kawaida.

“Sijaona sehemu yeyote bajeti hii inamtaja mfanyakazi, malalamiko ya watumishi wa umma ni mengi, mzigo wake mkubwa na hakuna nyongeza ya mshahara Mei Mosi imepita sijui kwanini wanamsahau mfanyakazi,” amesema Mwassa.

Martha Mlata, (Mbunge wa Viti MaalumCCM) amesema kitendo cha kuondoa ada ya magari kimewagusa wengi licha ya kodi kuongezwa kwenye mafuta anaamini kwamba gharama za maisha hazitakuwa kubwa kama wanavyosema watu wengine.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

Habari Mchanganyiko

“Jamii ielimishwe faida za uhifadhi”

Spread the loveWIZARA ya Maliasili na Utalii imesema ili kukabiliana na migongano...

Habari Mchanganyiko

Shahidi aeleza Nathwani alivyomshambulia jirani yake

Spread the loveSHAHIDI ambaye ni fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) ameileza mahakama...

Habari Mchanganyiko

DCEA, TAKUKURU waunganisha nguvu kupamba na dawa za kulevya, rushwa

Spread the love  MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya...

error: Content is protected !!