October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge waichachafya Serikali

Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa mjini

Spread the love

WABUNGE wamewasha moto kwa kuikosoa bajeti inayopendekezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, wakisema imejikita kuwakandamiza wananchi maskani huku ikikosa vyanzo vya uhakika vya mapato. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Moto huo wameuwasha wakati wakichangia hotuba iliyowasilishwa bungeni Ijumaa iliyopita na Saada Mkuya, Waziri wa Fedha na Uchumi ya Sh. 22.4 trioni.

Peter Msigwa wa Iringa Mjini (Chadema), amesema kupandisha kodi ya mafuta ya taa, petroli na dizeli ni kuwanyanyasa wananchi masikini.

Ameitaka serikali kuboresha sekta ya mtambuka ya utalii ambayo inachangia pato la taifa kwa asilimia 17. Kwamba ni hifadhi mbili za Serengeti na Kilimanjaro ndizo zinaweza kujiendesha kati ya hifadi 16.

“Tunapaswa kuwa makini katika uhifadhi. Tusipime uhifadhi kwa kuangalia fedha. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali amesema asilimia 20 ya fedha zinazotegwa huwa zinaliwa. Hivyo, hizo trioni 22.5 tunazotenga nazo zitaliwa,” amesema Msigwa.

Salehe Pamba wa Pangani (CCM), amesema elimu kuhusu ukusanyaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), inapaswa kutolewa kwa wafanyabiashara na wananchi. Pia lazima halmashauri zijengewe uwezo wa kukusanya angalau asilimia 10 ya kodi na serikali kuwa na kiwango cha ukomo cha kukopa katika taasisi za ndani ya nchi.

“Lazima tukope kiwango ambacho hakizuii wananchi na taasisi binafsi kukopa. Pia lazima kuwa na mipango mahususi kwa ajili ya kuondoa utegemezi kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 5 au kufuta kabisa utegemezi. Nchi ikijitegemea itapata heshima,” ameeleza Pamba.

Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Halfan Barwani (CUF), amesema “bajeti ya nchi ni tendo la kisheria. Siku za nyuma wananchi walihamasika kufuatilia bajeti. Lakini siku hizi wanaona ni tendo la kawaida.”

Amesema kwa sasa hata nusu ya bajeti haifiki kwa walegwa. Hakuna vyanzo vipya vya mapato. Bajeti si rafiki kwa maisha ya kawaida ya Watanzania wala mazingira ya nchi.

“Hakuna uwiano wa mgawanyo wa rasilimali. Bado vigezo sahihi vya upimaji wa mgawanyo wa bajeti havijawekwa. Tunataka serikali ya CCM ihakikishe mgawanyo sawa wa rasilimali hata kama ni kidogo.” Ameeleza Barwani.

 Naye Mohamed Sanya wa Mji Mkongwe (CUF), amesema hana tatizo na kuongezeka kwa bei ya mafuta. Ila ni busara kwa serikali kuangalia vyanzo vipya vya mapato.

“Serikali inapaswa kukusanya kodi ya majengo. Inaweza kupata asilimia tatu katika majengo ambayo hayalipiwi kodi kuliko kuhangaika na mafuta. Pia serikali ilipe deni ambalo shirika lake la ndege linadaiwa ili kuendelea kufanya biashara ya usafiri katika kanda na kimataifa kwa ajili ya kuongeza pato,” amesema Sanya.

Yeye Moses Machali wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), amesema serikali inapaswa kujiuliza ni sababu zipi zimepelekea kukua kwa uchumi wa Marekani ambapo kumepelekea kupanda kwa thamani ya Dola ya Marekani na kushuka kwa Shilingi ya Tanzania.

“Kuna mahali tunafanya uzembe kama taifa. Hata kama utakusanya fedha nyingi kiasi gani kama usimamizi wake ni mdogo, huwezi kuleta maendeleo. Serikali imeshidwa kuangalia sekta za utalii, uchukuzi na usafiri wa anga katika kuongeza mapato yake,” ameeleza Machali.

Suzan Kiwanga wa Viti Maalum (Chadema), amesema hakuna ongezeko lolote la bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16 kutoka bajeti ya mwaka 2014/15 kama ambavyo Waziri Mkuya ametoa taarifa yake wakati akisoma hotuba ya bajeti.

Amesema kushuka kwa shilingi na kupanda kwa thamani ya dola kunasababisha kutokuwepo kwa uharisia wa ongezeko la bajeti ya mwaka huu kwa sababu mwaka wa fedha uliopita dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa Sh. 1500 na kwa mwaka huu inanunuliwa kwa Sh. 2200.

“Mnapandisha bei ya mafuta ili kupeleka umeme vijijini. Umeme ambao hata wananchi wa kawaida vijijini hawautumii kutokana na gharama ambazo mnataka walipie. Gharama ya nguzo peke yake ni Sh. 500,000,” amefafanua Kiwanga.

error: Content is protected !!