WABUNGE wa viti maalum, wamehoji mkakati wa Serikali kupunguza gharama za matibabu ya ugonjwa wa figo ili kunusuru wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu hususani gharama za usafishaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akiuliza swali la msingi bungeni leo tarehe 21 Juni 2022, bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu, Mbunge Viti Maalum, Mariam Kisangi (CCM), amehoji; Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wagonjwa wa figo kupata matibabu ya kusafisha figo kwa gharama nafuu?
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema Serikali iko mbioni kukamilisha Muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote, ambayo itakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hilo.
“Mkakati wa Serikali katika kupunguza gharama za kusafisha figo ni kununua vifaa tiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, pia Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itakapokamilika itakuwa suluhisho la kudumu,” amesema Dk. Mollel.
Kuhusu wanaotumia bima za afya kutozwa fedha nyingi kupata huduma za kusafisha figo, Dk. Mollel amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, analifanyia kazi suala hilo na kwamba atatoa majibu kuanzia Julai Mosi, 2022.
“Waziri ameita timu kukaa chini kuangalia namna gani, sio tu kusaidia kwenye vifurushi vikubwa vya bima lakini hata wasio na bima ishuke kabisa hata ikiwezekana iwe Sh. 50,000 kwa mtu mmoja badala ya bei ya Sh. 900,000 kwa wiki ilivyo sasa. Waziri analifanyia kazi muda si mrefu tutapata majibu kuanzia Julai Mosi, 2022,” amesema Dk. Mollel.
Naye Mbunge Viti Maalum, Ghati Chomete, alihoji lini Serikali itapeleka mashine za kusafisha figo katika Hospitali ya Mwalimu Julius Nyerere.
Dk. Mollel amejibu akisema Rais Samia Suluhu Hassan amenunua mashine hizo 171, na kwamba hospitali hiyo itakuwa ni miongoni mwa hospitali zitakazonufaika na mgawo wake.
Kufuatia majadala huo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ameishauri Serikali kupunguza gharama za usafishaji figo kwa kuwa mashine zinanunuliwa na Serikali.
“Mnaponunua mashine Sh. bilioni moja, baada ya miaka miwili gharama inarudi kutokana na kuchangiwa. Hamuwezi mkawa mnapunguza gharama za matibabu sababu mashine zinachangiwa na matibabu?” amesema Zungu.
Leave a comment