SERIKALI imesema itatekeleza ahadi zote zilizotolewa na Rais wa awamu ya tano hayati Dk. John Magufuli ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami katika mji wa Bunda. Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).
Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Bunda mjini, Robert Maboto (CCM) leo tarehe 3 Septemba, 2021 jijini Dodoma, Naibu Waziri wa nchi, ofisi ya Rais TAMISEMI, David Silinde ahadi hizo zitatekelezwa kama Rais Samia alivyoahidi.
Katika swali la msingi, Maboto aliuliza “Je, ni lini serikali itatekeleza ahadi ya Rais wa awamu ya tano ya ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Bunda kwakuwa mpaka sasa hauna barabara za lami?”
Akijibu swali hilo katika kikao cha nne cha Bunge hilo la 12, Silinde alisema “Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) kutekeleza programu ya uendelezaji miundombinu katika miji unaotarajiwa kutekelezwa katika halmashauri za majiji, manispaa na miji 45 ikiwemo halmashauri ya Bunda mjini.
“Programu hii itahusisha pia ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Bunda kwa kuzingatia vipaumbele vitakavyoainishwa na halmashauri ya Bunda mjini.
“Serikali itatekeleza ahadi zote za Rais Magufuli kama ilivyoahidiwa na Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan katika hotuba aliyotoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021.”
Naibu waziri huyo pia ameitaka halmashauri ya Bunda kuweka vipaumbele vya miundombinu wanayotaka serikali ishughulikie ikiwemo ujenzi wa soko kuu la Bunda pamoja na stendi mpya ikiwa ni miongoni mwa ahadi alizozitoa Rais.
Leave a comment